Na Israel Mwaisaka
Nkasi
MAHAKAMA
ya wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa imemuhukumu kutumikia kifungo cha miaka
30 jela, Jovin Bukambo (30) mkazi wa kitongoji cha Nkomolo wilayani
Nkasi kwa kosa la kujaribu kumbaka Bibi kizee Maria Tenganamba (60).
Akisoma hukumu hiyo jana, Hakimu mkazi wa mahakama hiyo Ramadhani
Rugemalila alisema mahakama hiyo imeridhishwa na ushahidi pamoja na maelezo ya upande wa mashitaka
pasipo kuacha shaka yoyote na kumtia hatiani mtuhumiwa huyo ndipo alipotoa hukumu hiyo ya miaka 30 jela kwa kuzingatia kifungu
Na,132 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka wa
2002.
Awali mwendesha mashitaka wa polisi Hamimu Gwelo
aliieleza mahakama hiyo kuwa mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo Oktoba 16 mwaka
jana nyumbani kwa Bibi huyo maeneo ya Nkomolo wilayani Nkasi majira ya saa 11
jioni ambapo mtuhumiwa alimvamia bibi huyo na kutaka kumbaka.
Alisema akiwa katika jaribio hilo kabla ya kufanikiwa
kutekeleza kosa hilo Bibi huyo alipiga kelele na kuokolewa na baadhi ya vijana
waliokuwa karibu na eneo hilo ndipo walipofanikiwa kumkamata kijana huyo akiwa uchi na
kumfikisha Polisi.
Upande wa mashitaka uliwakilishwa na mashahidi watatu ambao
walitoa ushahidi ambao haukuwa na mashaka wakati mtuhumiwa alijitetea
mwenyewe.ambapo aliiomba Mahakama impunguzie adhabu kutokana na kwamba amekaa
muda mrefu Mahabusu na anategemewa katika familia yao.
Upande wa jamhuri uliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali
kwa mtuhumiwa ili iwe fundisho kwa watu wengine, ndipo mahakama hiyo iliamua kutoa adhabu
ya miaka 30 jela ikizingatia ombi la jamhuri kwa nia ya kukomesha vitendo hivyo.
No comments:
Post a Comment