Thursday, 11 May 2017

Mlele wadai walikuwa hawajui kama miradi ya maji inawahusu

Na Gurian Adolf
Mlelele

MIONGONI mwa changamoto zinazo ikabili Halmashauri ya wilaya ya Mlele mkoani Katavi katika suala zima la kutoa huduma ya maji safi kwa wananchi wa wilaya hiyo ni uchakavu wa miundombinu ya maji sambamba na uelewa mdogo katika masuala mbalimbali ikiwemo kuchangia huduma za maji safi na usafi wa mazingira wilayani humo.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo Deusi  Bundala  wakati akifunga mafunzo ya siku tatu  kwa viongozi wa kata na vijiji yaliyokuwa na lengo la kuwajengea uwezo juu ya utunzaji  wa miundombinu ya maji katika maeneo yao wilayani humo.
Alisema kuwa wananchi halmashauri hiyo bado wana dhana kuwa Serikali ndiyo yenye jukumu la kuwajengea miundombinu ya maji na hivyo wao kama wananchi hawawajibiki kwa lolote huku wakisubiri tu kutumia huduma za maji safi.

Alisema kuwa pamoja na kuwepo kwa dhana hiyo bado serikali imekuwa ikijitahidi kujenga miundombinu hiyo lakini hata kuisimamia na kuifanyia ukarabati pindi inapokuwa imechakaa wanaona hawahusiki na hivyo kuiacha ikiwa imechakaa na wao ndiyo wanao teseka kwa kukosa huduma hiyo muhimu ya maji.

Kupitia mafunzo hayo wananchi hao wameweza kufahamishwa kuwa wao ndiyo wadau namba moja wa maendeleo katika mazingira yao kwani miradi mbalimbali inayotekelezwa na serikali ni jukumu lao kuitunza kwani inapo haribika wao ndiyo wanao pata shida kutokana na kuharibika huko.

Aidha mwenye kiti huyo wa halmsahauri aliwaambia kuwa ni jukumu lao kuisimamia na kuitunza na kuifanyia matengenezo miradi mbalimbali iliyipo wilayani humo ambayo imetekelezwa na serikali kwani inawafaa wao lakini kuiacha ikiharibika kana kwamba haiwahusu mwisho wa siku wahao hangaika ni wao wenyewe.
Kwaupande wake mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii,Elimu, Afya na Maji wa baraza la madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mlele Leonard Kiyungi alikiri kupwepo kwa suala la wananchi kutumia vibaya miundombinu ya maji na wakati mwingine  kuitelekezea Serikali pindi inapoharibika hali iliyosababisha Halmashauri kutoa huduma ya maji chini ya kiwango.
Mmoja wa wakazi wa kijiji cha Nsekwa wilayani humo, Bernadeta John  akichangia mada katika mafunzo hayo alisema kuwa wao wanachojua ni kuwa miradi yote ya Serikali ni lazima ihudumiwe na serikali ikiwemo ni pamoja na utunzaji wake lakini kutokana na mafunzo waliyoyapata hivi sasa watabadirika na kuiona ni mali yao.

Naye Yahaya Mpenda Mwenyekiti wa kijiji cha Kalovya kata ya Inyonga Wilaya ya Mlele amesema kuwa yeye atahakikisha  katika kijiji chake  wananchi wanachangia ili waanzishe mfuko wa maji wa kijiji  fedha ambazo zitatumika katika kufanya matengenezo ya miundombinu ya maji pindi miradi  inapoharibika na kuachana na dhana ya kuisubilia Serikali ifanye kazi hiyo.
Kutokana na maamuzi hayo mhandisi wa Maji wa halmashauri ya Wilaya ya Mlele Boniphace Mapambano amewapongeza viongozi wa ngazi za kata na vijiji kwa kuitikia wito wa kuhudhuria mafunzo ya kuwajengea uwezo katika miradi ya maji na kuazimia kubadirika na kuachana na mtazamo waliokuwa nao awali kwani sasa wametambua kuwa miradi hiyo wao ndiyo wamiliki kwani inawafaa wao wenyewe.
 
Halmashauri ya wilaya ya Mlele ni miongoni mwa halmashauri tano katika mkoa wa Katavi ambayo ilianzishwa baada ya kugawanywa kutoka katika iliyokuwa Halmashauri ya Mpanda ambayo sasa inafahamika kama Halmashauri ya wilaya ya  Tanganyika.
Hivi sasa Halmashauri hiyo  kwa kushirikiana na Serikali kuu imefanya ukarabati wa visima hamsini na tisa (59) na kujenga visima vipya21 na kufanya upatikanaji wa huduma ya maji kufikia asilimia hamsini na sita (56%) mpaka mwezi Mei mwaka huu.
Katika halmashauri hiyo hivi saa inatekelezwa miradi ya kujenga Pumping Schemesza kisasa katika vijiji vya Nsenkwa,Mapili,Ilunde,Wachawaseme,Kamsisi na Mji wa Inyonga ili kumaliza tatizo la ukosefu wa maji safi katika wilaya hiyo.
Mwisho

No comments:

Post a Comment