Thursday, 11 May 2017

Rukwa na Katavi washauriwa kujenga hotel zenye hadhi ya nyota 5

Na Gurian  Adolf
Sumbawanga
 
SERIKALI imesema kuwa siyo kazi yake kujenga hotel za kifahari zikiwemo zenye hadhi ya nyota tano bali ni kutengeneza mazingira kwa wawekezeji mbalimbali wakiwemo wa mahoteli ya aina hiyo ili waweze kujenga hoteli hizo ziweze kuvutia watalii wanaofika hapa nchini.

Hayo yamebainishwa Jana(Leo) bungeni na naibu waziri wa Maliasili na utalii Mahmood Mgimwa wakati alipokuwa  akijibu swali la  mbunge wa mkoani Katavi Tasca Mbogo aliyetaka kufahamu ni lini serikali itajenga mahoteli ya kifahari ikiwemo yenye hadhi  ya nyota tano  ambayo wataweza kufikia  watalii pindi watakapo  kuwa wanakwenda  kufanya utalii katika mkoa huo.

Akijibu swali hilo naibu waziri  huyo alisema kuwa siyo kazi ya serikali kujenga hotel bali  kazi ya serikali ni kutengeneza Mazingira ambayo yatawawezesha wawekezaji wa ndani na nje ya mkoa huo ili waweze kuwekeza katika sekta ya utalii ikiwemo ujenzi wa hoteli  hizo.

Alisema kuwa nivizuri sasa kwa wakazi wa mikoa ya Rukwa na Katavi kutumia fursa hiyo  kujenga hotel za kitalii ikiwemo na vitu vya aina  mbalimbali kama viwanja vya michezo, mabwawa ya kuogelea pamoja na hospital za kisasa ambazo  zitasababisha watalii watembeleapo vivutio vya utalii vikivyopo katika mikoa hiyo wajione wako katika Mazingira ya kuvutia na yenye huduma zote za muhimu.

Alisema kuwa ni ukweli usiopingika kuwa mikoa hiyo hivi sasa inafunguka kwakua serikali imejenga uwanja wa ndege wa kisasa katika mkoa wa Katavi na hivi sasa inaendelea kujenga barabara  kwa kiwango cha lami zinazoingia na kutoka katika mikoa hiyo hivyo ni wazi  kuwa watalii wengi  watakuwa wana kwenda kutembelea  katika mikoa hiyo.

Mgimwa alisema kuwa wananchi wa mikoa hiyo wanapaswa kuchangamkia fursa hiyo na waweze kuwekeza ili waweze kufanya biashara sambamba na kutoa ajira ambazo  zitapatikana kupitia uwekezaji  katika sekta ya utalii.

Hata hivyo alisema bado wanaweza  kualika wafanyabiashara wakubwa wa nje ya nchi na wakawekeza ambapo watasaidia kuongeza  ajira kwa watanzania ambao wataajiriwa katika mahoteli ama kupitia sekta hiyo ya utalii.

Mikoa ya Rukwa na Katavi inafursa  nyingi za utalii ikiwemo ni pamoja na hifadhi ya Taifa  ya Katavi, wanyama wa aina mbalimbali, mapori ya akiba, Maporomoko ya maji ya mto  Kalambo, Chemchemi za maji ya moto na vingine vingi  ambavyo  bado havijatangazwa na vinaweza kuliingizia taifa  fedha za kigeni kutokana na biashara ya utalii.

Mwisho

No comments:

Post a Comment