Friday 28 April 2017

Ndugu wasusa kuchukua maiti ya marehemu wakishinikiza uchunguzi wa kina ufanyike

Na Gurian Adolf
Sumbawanga

NDUGU wa marehemu Juma Dereva(38) jana walisusia kuchukua maiti ya ndugu yao huyo kwa Madai kuwa wanaamini  kuwa kifo chake kimetokana na kipigo kutoka kwa Askari polisi wa kituo cha Mpui wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa.

Akizungumza na rukwakwanza.blogspot.com mmoja wa ndugu hao Daniel Mohammed mkazi wa kijiji cha Malolwa wilayani humo alisema kuwa wao wamesusia kuchukua mwili wa marehemu wakidai kuwa wanataka  uchunguzi wa kitabibu ufanyike kwakua kifo cha ndugu yao huyo kilikuwa ni cha ghafla na alikua haumwi.

Alisema kuwa tukio la  kifo hicho lilitokea April 26 majira ya saa  9 za mchana kwani ndugu yao huyo ambaye yeye ni baba yake  mdogo alitoka nyumbani kwake na kuwapelekea chakula  mtoto wake aitwaye Loyce Mohammed pamoja na mume wake Leonard Kaembe waliokuwa  wanashikiliwa na polisi katika kituo hicho cha Mpui.

Alisema kuwa wanandoa hao walikuwa na ugomvi baina yao ambapo jirani yao aliyefahamika kwa jina  moja la Melkio akiwa na mtoto wake Lazaro Melkio walikwenda  kuwaamua na kisha wanandoa hao waliacha kupigana wakaanza kumpia Mzee Melkio hadi kumvunja mguu.

Baada ya kumvunja mguu alikwenda polisi na kupewa PF3 na kisha kwanza kupatiwa matibabu katika kituo cha afya cha Mpui kilichopo wilayani humo.

Siku iliyofuata Juma Dereva aliwapelekea chakula  watuhumiwa na kwenda kuwawekea dhamana ambapo alipelekwa na bodaboda mpaka kituo cha polisi.

Baada ya saa  nzima  mmoja kati ya ndugu wa marehemu alipigiwa simu na muendesha bodaboda akiwaarifu kuwa ndugu yao aliyempeleka katika kituo cha polisi amefariki dunia.

Aliwaeleza kuwa mtoto wa mzee Melkio aliyefunjwa mguu baada ya kumuona marehemu akiwapelekea chakula  watuhumiwa aliwafuata na kuwaeleza askari polisi kuwa naye aliwlmtishia maisha hali iliyopelekea askali polisi kumkamata na kumuingiza mahabusu.

Alisema baada ya kumuingiza mahabusu alianguka chini na kufariki dunia ndipo  yeye alipoamua kuwapigia simu kuwaarifu ndugu zake kuwa Dereva amekufa.

Polisi baada ya kuona ameanguka walimchukua na kumpeleka katika kituo cha afya cha Mpui lakini mganga liyempokea aliwaambia kuwa amekwisha fariki dunia.

Ndipo  ndugu wa marehemu huyo walipofika katika chumba cha kuhifadhia maiti wakiwa na diwani wa Kata ya Mpwapwa Abel Msumbachika ambaye alisema kuwa mwili wa marehemu ulikuwa na jeraha kichwani huku vishikizo vya shati vikiwa vimekatika hali ambayo ilisababisha ndugu wa marehemu kupata mashaka ndipo  walipoamua kugoma kuchukua mwili huo wakidai kuwa wanataka  kwanza uchunguzi ufanyike.

Diwani Msumbachika alisema kuwa kufuatia Madai hayo mwili wa marehemu ulisafirishwa kupelekwa katika hospitali ya mkoa wa Rukwa ili uchunguzi ukafanyike kwa lengo la  kuweza kujua sababu hasa  za kifo cha marehemu.

Kwaupande wake kaimu kamanda wa jeshi  la  polisi mkoani Rukwa Polycarp Urio alipozungumza na rukwakwanza.blogspot.com  alikiri kuwepo kwa tukio la  mtu kufa  lakini alisema kuwa bado uchunguzi unafanyika kuhusiana na tukio hilo.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment