Friday 28 April 2017

Ulevi wa kupindukia wasababisha afisa mtendaji wa kijiji kusimamishwa kazi

Israel   Mwaisaka
Nkasi

MKURUGENZI wa halmashauri ya wilaya Nkasi Julius Kaondo amemsimamisha kazi afisa mtendaji wa kijiji cha Kakoma kata ya Kipundu wilayani Nkasi mkoani Rukwa Alphonce Mseo baada ya kubainika kushindwa kutekeleza majukumu yake ya kikazi kutokana na ulevi wa kupindukia.

Hatua hiyo imekuja baada ya mkuu wa wilaya Nkasi Said Mtanda kufika katika kijiji hicho kufuatilia maagizo ya serikali ya ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa agizo ambalo halijatekelezeka ikiwa ni pamoja na kumkuta mtendaji huyo wa serikali akiwa amelewa pombe kupindukia muda wa kazi.

Akitoa taarifa kwa Waandishi habari jana mkurugenzi wa wilaya hiyo alidai kuwa Wananchi wamekua wakimlalamikia afisa huyo wa kijiji juu ya uwezo wake wa kufanya kazi iliyopelekea hata maendeleo ya kijiji kushindwa kupiga hatua licha ya kwamba wamekua wakitoa michango mbalimbali ya kijiji.

Alisema kuwa kutokana na malalamiko hayo na kubaini kuwa ulevi wa kupindukia umepelekea kupunguza uwezo wa mtumishi huyo wa Umma kupotea alimuamuru mkurugenzi wa wilaya kumsimamisha kazi mtendaji huyo wa kijiji ili kupisha uchunguzi juu ya tuhuma hizo zinazomkabili.

Kaondo alisema kuwa baada ya tuhuma hizo afisa mtendaji huyo wa kijiji alitakiwa ajieleze juu ya tuhuma hizo zinazomkabili za kukusanya michango kwa Wananchi lakini hakuna maendeleo yoyote yanayofanywa hasa ya ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa na ulevi wa kupindukia ambapo mtendaji huyo alishindwa kujitetea ipasavyo.

Amefafanua kuwa halmashauri itampeleka mkaguzi wa ndani wa halmashauri kwenda kukagua mahesabu katika kijiji hicho na ikibainika kuwa kuna kasoro mtendaji huyo atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zitakazokuwa zikimkabili.

Halmashauri itampeleka mara moja afisa mtendaji mwingine wa kijiji kwenda kushirikiana na serikali ya kijiji hicho kusukuma maendeleo ya kijiji hicho mbele.

Alipohojiwa na gazeti hili kuhusu tuhuma hizo alisema kuwa hana cha kuzungumza zaidi bali anasubiri tu taarifa ya uchunguzi pale itakapokamilika.
Mwisho

No comments:

Post a Comment