Monday 24 April 2017

Mtoto afichwa ndani kwa miaka nane kwasababu ni mlemavu

Gurian  Adolf
Sumbawanga

MTOTO  Hapness Churura(8) ambaye ni mlemavu wa viungo  hajawahi kutolewa nje kwa kipindi cha maisha yake yote tangu kuzaliwa kwake kutokana na wazazi wake kuwa wanamficha ndani wakidai kuwa wanaona aibu kwa jamii kutokana na kuwa na mtoto  mlemavu.

Mtoto huyo  yupo katika Kijiji cha Chala C wilayani Nkasi mkoani Rukwa amekua akifichwa ndani na wazazi wake na akipewa huduma zote za kibinadamu humo ndani lakini  hawakuweza kumtoa nje hata kuota jua kutokana na kuona aibu familia hiyo kuwa na mtoto  mremavu. 

Mmoja wa wakazi wa kijiji hicho Edwin Mselema akizungumza kwa njia ya simu na mwandishi wa habari hii alisema kuwa kitendo walichokifanya wazazi hao in kibaya na si  cha kiungwana kinachopaswa kukemea na jamii nzima  ya kijiji hicho.

Alisema kuwa kitendo hicho kimemnyima fursa nyingi mtoto huyo ikiwemo ni pamoja na kusaidiwa na wakazi wa kijiji hicho, watu wengine wasamaria wema pamoja na serikali kupitia mfuko wa maendeleo vijijini TASAF.

Mselema alisema kuwa kitendo cha kumfungia ndani kimekiuka haki zake za msingi kama kupata elimu, matibabu, kucheza na nyinginezo na hii inatokana na baadhi ya watu kutokuwa na elimu dhidi ya watu Wenye ulemavu.

Alisema mtoto  Hapness amekuwa ni mremavu wa kulala kitandani kwa muda wote tangu  azaliwe kiasi kwamba amedhoofu afya yake  kwa kutotoka nje kupata jua pamoja na hewa na wakati mwingine kukosa mtu  wa kumgeuza alipolala pindi wanafamilia hiyo wanapokuwa wametoka kwenda kwenye shughuli zao.

"Sasa wazazi wanahangaika kumlea kwa shida peke yao, wakati kama ingefahamika kuwa wanamtoto mlemavu wangeweza kusaidiwa, hali ambayo inawazidishia ugumu wa maisha na usumbufu wa kumficha mtoto  huyo  wakati si  kosa kuwa na mtoto  mlemavu kwani ni mapenzi ya Mungu"... Alisema.

Alisema kuwa bado serikali kupitia vyombo vya habari, pamoja na mashirika ya ndani na nje yanawajibu wa kutoa elimu ili jamii iwachukulie watu Wenye ulemavu kuwa ni  binadamu wanaostahili haki zote hivyo  kuwaficha ndani ni makosa.

Mkazi huyo wa kijiji cha Chala ambaye ni mdau wa masuala ya habari kijiji hapo alisema kuwa jamii nayo  inakua haijihusishi kujua kuhusu maisha ya watu wengine kwani mama wa mtoto  hiyo alibeba ujauzito lakini  hawakujiuliza hatma ya ujauzito ule ulikua ni ni ni kwani hawaoni mtoto wala hakukua na taarifa kuwa mwanamke huyo  amejifungua maiti, ama  mtoto  alifariki baada ya kuzaliwa.

" Najaribu kuvuta taswira hivi ingetokea mtoto  huyo  amefariki inamaana wangeweka msiba, ama  wangeenda kuzika usiku, mama wangeutupa mwili wake porini maana kijijini watu walikuwa hawana taarifa za kuwepo kwa mtoto  hiyo mpaka Jana ambapo imefahamika sijui nini  kingetokea iwapo mauti yangemfika mtoto  huyo" ... Alisema Maria Kasamya huku akiangua kilio kwa uchungu.

Naye Coleta Kachonta mkazi wa kijiji hicho alisema kuwa huo ni ukatili wa haki ya juu aliofanyiwa Hapness ambao inapaswa hatua za kisheria zichukuliwe kwa wazazi wake ili wananchi wengine wajifunze kupitia tukio hilo ambalo limesababisha mateso makubwa kwa takribani miaka 8 ya mtoto  huyo  tangu  kuzaliwa kwake.

Naye Mwenyekiti wa kijiji hicho John Kapongwa akizungumza kwa njia ya simu alisema kuwa hata  yeye anashaa kuwepo kwa mtoto  huyo katika kijiji hicho kwani walikuwa hafahamu kabisa ila anashangaa na aliwashukuru majirani waliosababisha kujulikana kuwepo kwa mtoto  huyo.

Alisema kuwa itabidi serikali ya kijiji ifanye kila liwezekanalo ili tabia  hiyo ikomeshwe katika kijiji hicho na kutafuta watu waweze kutoa elimu ili jamii ibadilishe dhana  potofu waliyokuwa nayo  dhidi ya watu Wenye ulemavu.
Mwisho

No comments:

Post a Comment