Sunday 23 April 2017

Auawa kwa kukatwa mapanga kutokana na imani za kishirikina

Israel Mwaisaka
Nkasi

 MKAZI mmoja wa kijiji cha Mwenge kata ya Kate wilayani Nkasi mkoani Rukwa Joseph Songaleli (56) amefariki dunia baada ya kuuwawa kinyama na watu wasiofahamika

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa kijiji hicho Medadi kitinsi alisema kuwa marehemu huyo alivamiwa nyumbani kwake usiku wa kuamkia juzi majira ya saa sita usiku ambapo watu watano wenye silaha za jadi waliuvunja mlango wa nyumba ya marehemu kwa kutumia jiwe kubwa aina ya Fatuma ambapo waliingia na kuanza kumshambulia mtu huyo.

Alisema awali mke wa marehemu baada ya mlango kuvunjwa alitokea dirishani na kukimbia na ndipo wauaji hao walipopata nafasi ya kumkamata mume wake na kuanza kumshambulia kwa silaha hizo za jadi ikiwemo marungu na mapanga.

Alidai kuwa kulitokea mapambano makali kati yao ambapo marehemu alijitahidi kujiokoa lakini alizidiwa nguvu na akaamuliwa alale kifudifudi na ndipo alipoanza kukatwa mapanga kichwani hadi walipo muua.


Mwenyekiti huyo wa kijiji amedai kuwa mauaji hayo chanzo chake kikuu ni imani za kishirikina ambapo inasemekana marehemu aliingia mgogoro na mmoja wa ndugu zake akidai kuwa marehemu alikua akimroga .

habari za Kipolisi zinadai kuwa mpaka sasa wanamshikilia mtu mmoja kuhusika na tukio hilo na kuwa uchunguzi zaidi unaendelea ili kuweza kuwakamata wale wote waliohusika katika tukio hilo.

Mkuu wa wilaya Nkasi Said Mtanda amesikitishwa na mauaji hayo ambayo chanzo chake kikuu ni imani za kishirikina na kuwa serikali inachokifanya ni kuhakikisha wale waliohusika wanakamatwa na sasa wataanza kupita kila kijiji na kuanza kuielimisha jamii juu ya kuachana na imani hizo potofu.
Mwisho

No comments:

Post a Comment