Sunday 30 April 2017

Maafisa 171 wa TANAPA wahitimu mafunzo ya jeshi usu

Walter Mguluchuma
Katavi
Jumla ya Askari 171 wa  Hifadhi za Taifa za TANAPA na wamamkaka ya Hifadhi ya Ngorongoro wamehitimu mafunzo ya awali ya utendaji wao wa kazi wa kutoka mfumo wa kiraia na kuwa jeshi usu(para millitary) .

Mafunzo hayo ya mwezi mmoja na nusu yalifungwa  jana na Mkuu wa Mkoa wa Katavi Meja Generali mstaafu Raphae Muhuga katika kituo maalumu cha mafunzo cha Mlele kilichopo Mkoani Katavi.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA Mtango Mtahiko alisema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwaandaa wahitimu hao kufanya kazi kutoka kwenye utendaji wao wa kazi wa sasa na kufanya kazi kwa mfumo wa kijeshi ili kuweza kulinda mali asili za nchi na kujilinda wao wenyewe dhidi ya majangiri.

Alisema mafunzo hayo yatasaidia kuwafanya asaskari hao na wale ambao wameisha pata mafunzo kama hayo kwenye kituo cha mafunzo cha Mlele kubadilika katika utendaji wao wa kazi na yatasaidia kutatua matatizo yaliopo ya ujangili na uhifadhi wa mazingira .

Mtahiko alieleza kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii Profesa  Jumanne Magembe ameisha agiza kuwa katika kuelekea mfumo wa utendaji kazi wa kutoka urai na kuwa jeshi usu ni lazima watumishi wote waliochini ya Wizara hiyo kupitia mafunzo kama hayo katika kituo hicho cha mafunzo cha Mlele.

Meneja wa ulinzi wa TANAPA Massana Mwishawa alisema malengo ya kufanya mafunzo hayo ni kuwatoa askari hao kwenye mfumo wa kiraia na kwenda kwenye mfumo wa kijeshi.

''lengo kubwa ni kuhahakikisha maliasili za nchi zinakuwa salama na mafunzo hayo yatakuwa ni endelevu ili kuweza kukabiliana na changamoto za sasa za ujangili na uingizwaji wa mifugo ndani ya Hifadhi''...alisema

Akitoa taarifa ya mafunzo hayo Fidelis Kapalata alisema kuwa mafunzo hayo yaliwashirikisha wahitimu 171 kati yao watano walikuwa ni wahifadhi na 166 ni askari wa daraja la pili ambapo askari watatu walifukuzwa kituoni hapo kwa utovu wa nidhamu .

Alisema wahitimu hao wamepatiwa mafunzo ya vitendo na nadhalia hivyo yatawafanya wafanye kazi kwa ufanisi zaidi na endapo watapata ushirikiano kwa wananchi ujangili utakua ni ndoto hapa nchini .

Nae msoma risala ya wahitimu wa mafunzo hayo Nowa Rael alieleza kuwa wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya kutopandishwa vyeo kwa wakati kwani wengi wa askari hao hawaja pandishwa vyeo kwa kipindi cha muda mrefu sasa.

Pia waliomba kituo hicho kiboreshewe miundo mbinu ya maji na barabara pamoja na mawasiliano ya simu kwani kituo hicho hakina mawasiliano ya simu.

Mkuu wa Mkoa wa Katavi Meja Generali Mstaafu Raphael Muhuga alisema kuwa mfumo ambao wanataka kuingia wa jeshi usu sio mgeni kwani zipo baadhi ya nchi zinatumia mfumo huo kwa muda mrefu sasa na zimefanikiwa.

Kwa upande wa changamoto ya mawasiliano ya simu alisema atafanya mawasiliano na makampuni ya simu ili kuona uwezekano wa kuweka mawasiliano ya simu kwenye kituo hicho.

Mwisho

No comments:

Post a Comment