Sunday 30 April 2017

Wenyeviti wa vijiji laamani kwa kushiriki ujambazi

Gurian Adolf
Sumbawanga. 

Imeelezwa kwamba asilimia kubwa ya wenyeviti wa Serikali za vijiji wilayani Tarime mkoani Mara wanajihusisha na matukio ya ujambazi hali ambayo inafanya jamii kwa kushirikiana na vyombo vya dola kupata wakati mgumu kudhibiti uhalifu.

Katibu wa Muungano wa Jamii Tanzania (MUJATA) Peter Kayemba Mpeleka alisema hayo jana wakati akizungumza na viongozi wa dini za kikristo kutoka makanisa mbalimbali ya mkoa wa Rukwa, kikao kilicholenga kuutambulisha muungano huo kilichofanyika katika ukumbi wa Kanisa la FPCT mjini hapa.

Alisema pamoja na jitihada za Muungano wa Jamii Tanzania kwa kushirikiana na vyombo vya dola kupambana ili kudhibiti uhalifu lakini imekuwa vigumu kwa wilaya ya Tarime kwa kuwa asilimia kubwa ya viongozi wa vijiji na mitaa wamekuwa wakijihusisha katika matukio ya ujambazi wa kutumia silaha.

"Tarime ni vigumu kudhibiti uhalifu kwani wenyeviti na wajumbe wa serikali za vijiji ndio majambazi kwa hiyo hata tukitaka kufanya utambuzi wa wahalifu ili tuweze kuwadhibiti viongozi hao hawatoi ushirikiano kwa sababu nao ni sehemu ya majambazi" alisema.

Hata hivyo, Mpeleka aliongeza kwamba Muungano huo ambao una nia ya kuhakikisha jamii inakuwa na amani nyakati zote umeanza kuwaelimisha wakazi wa Tarime kuacha kutembea na mapanga na Sime kitu ambacho wameanza kufanikiwa.

Alisema kupitia MUJATA itazaliwa Muungano wa jamii mkoa wa Rukwa ( MUJARU) ambayo itakuwa na jukumu la kudhibiti uhalifu na vitendo vya kishirikina vinavyosababisha kutokea kwa mauaji ya mara kwa mara hasa katika maeneo ya vijijini.

Alisema jukumu la kudhibiti mauaji hayo si la vyombo vya dola pekee hivyo muungano huo ambayo viongozi wa madhebu ya dini watashirikishwa ndio itakuwa ni moja ya kazi yake.

Naye, Mchungaji Jacob Silungwe alisema viongozi wa dini wanaunga mkono wazo la mkoa huo kuanzisha muungano huo kwa kuwa hawaendi kinyume na sheria na taratibu za nchi.

Alisema pia wanatarajia utakuwa chachu ya kupatikana kwa amani na kupunguza si tu matukio ya mauaji ya kishirikina na uhalifu miongni mwa jamii.

Mwisho.  

No comments:

Post a Comment