Tuesday 12 April 2016

Wafugaji Mlele wamuangua DC

Na Gurian  Adolf
Mlele
WAFUGAJI wilayani Mlele mkoani Katavi wamemuangukia mkuu wa wilaya hiyo Issa Njiku wakimuomba asitishe kwanza  agizo lake la kuwataka waondoke katika mapori wanapofugia kwa madai kuwa maeneo hayo ni mapori tengefu.

Akiongea na  waandishi wa  habari  jana  mwenyekiti wa Chama  cha  wafugaji mkoa  wa  Katavi  (CCWT) Mussa  Kabushi  alisema   chama  cha wafugaji kinamwomba  mkuu huyo wa  Wilaya  asitishe  zoezi  alilopanga lianze kufanyika   Aprili  20  katika  Kata ya  Ugala  la kuwahamisha  wafugaji waliofuga mifugo  katika  mistu ya   Kata ya Ugala  katika  vijiji vya  Katambike  Kamili  na Kitongoji   Sanda.

Alisema kutokana na agizo la mkuu huyo wa wilaya la kuwataka wafugaji waondoke katika maeneo waliyopo hivi sasa linawasababishia usumbufu mkubwa na kuwafanya wajihisi kana kwamba wananyanyasika ndani ya nchi yao na wamekuwa wakifukuzwa fukuzwa hovyo bila utaratibu kama ni wakimbizi walioko ugegenini.

Kabushi alisema kuwa katika wilaya hiyo kuna mgawanyo wa matumizi ya ardhi ambapo
eneo walilotengewa wafugaji  ni  Ekta 3,765 sawa  na  hekta 9,430 ambalo linatosha  kulishia  mifugo   1,886 wakati  mifugo  iliyopo ni  zaidi ya  elfu  kumi .

Alisema kutokana na kutokuwa na eneo la kutosha kumesababisha wafugaji kuchungia mifugo hadi nje ya eneo walilotengewa hatua ambayo inatafsiriwa na serikali ya wilaya kuwa wamevamia katika maeneo ya hifadhi na hivyo kufukuzwa bila hata majadiliano.

Mwenyekiti huyo wa wafugaji alisema kuwa kwakuwa wakati mchakato wa ugawaji maeneo hayo unafanyika wafugaji hawakushirikishwa ni vizuri buasra za mkuu wa wilaya zikatumika na akaitisha mkutano ili zoezi hilo lifanyike upya kwa kuwashirikisha wafugaji ili kuondoa hata hatari ya mivutano baina ya wafugaji na wakulima.

Hivi karibuni Kwenye  mkutano  wa hadhara katika kata ya Ugalla wilayani humu,mkuu  huyo wa  Wilaya aliagiza ifikapo April 20 wafugaji wote wanaochungia ng'ombe katika hifadhi na maeneo mengine ambayo ni tengefu  waondoke mara moja  pia  aliwataka  wafugaji hao wapunguze mifugo yao ambapo aliwasahauri  waipunguze hadi kufikia mwenye ng'ombe 200 abaki na 100 na mwenye 100 abaki na 50.

Mwisho

No comments:

Post a Comment