Tuesday 12 April 2016

Dc Sumbawanga aagiza baa kufunguliwa jioni

Na Gurian  Adolf
Sumbawanga

MKUU wa wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa Methew Sedoyeka amepiga
marufuku biashara ya  kuuza pombe na vilevi vingine nyakati za asubuhi
badala yake biashara hiyo ianze kufanyika kuanzia saa 9;00 za mchana
baada ya muda wa kazi.

Akizungumza na vyombo vya habari ofisini kwakwe Methew Sedoyeka
alisema kuwa biashara hiyo imekuwa ikisababisha watu kunywa pombe
asubuhi na kushindwa kufanya kazi hali inayowasababisha washindwe
kujipatia kipato.

Alisema haiwezekani wilaya hiyo ikawa na walevi wengi kupita
wazalishaji kwa kufanya kazi na hivyo ameviagiza vyombo vya ulinzi na
usalama vya wilaya kuhakikisha vinachukua hatua kwa watu watakao kaidi
amri hiyo ya DC.

Aidha alitoa wito kwa wananchi wa Manispaa ya Sumbawanga pamoja na
wilaya ya Sumbawanga kujituma katika kazi ili waweze kupata kipato
kikubwa kitakacho wawezesha kujipatia maendeleo kutokana na nguvu kazi
yao.

Baadhi ya wakazi wa mji wa Sumbawanga wamepokea kwa mtazamo tofauti
agizo hilo la mkuu wa mkoa ambapo baadhi yao wamepongeza agizo hilo
huku wengine wakilalamikia kwamadai kuwa wao uzalishaji wao unatokana
na kuuza  vilevi na wanalipa kodi.

Mmiliki mmoja wa baa mjini humu Peter  Kayanda alisema kuwa wapo watu
kazi zao wanafanya nyakati za usiku kama walinzi na waliopo zamu za
usiku kazini muda wao wa kupumzika na kupata starehe unakuwa ni
asubuhi jioni ni muda wa kuelekea kazini.

Alisema kuwa pia serikali inapaswa kufahamu kuwa makampuni yanayouza
vilevi hapa nchini ndiyo yanaongoza kwa kulipa kodi tofauti na
makampuni ya uchimbaji wa madini hatua hiyo inaweza kusababisha
kupungua kwa mapato hata ya serikali.

Naye Monica Mayage mkazi wa Sumbawanga alisema kuwa kitendo hicho
kitasababisha pia watumishi walevi wa sekta binafsi na serikali kuwepo
kazini muda wote wa kazi na kuwajibika kwani baadhi yao wamekuwa
wakitoroka hata kazini kwajili ya kwenda kunywa pombe.

Mwisho

No comments:

Post a Comment