Tuesday 12 April 2016

Serikali ya kijiji yawaonya wafugaji kutembea na silaha za jadi



Na Gurian Adolf
Nkasi.

SERIKALI ya kijiji cha Ntatumbila wilayani Nkasi Mkoani Rukwa imewapiga marufuku watu wa jamii ya wafugaji kwenda maeneo ya starehe wakiwa na silaha za jadi ikiwemo mapanga hali ambayo inahatarisha usalama wa eneo husika.

Mwenyekiti wa kijiji hicho Ignas Kanjele alipiga marufuku hiyo katika mkutano wa kijiji uliofanyika jana uliokuwa na lengo la kuzungumzia hali ya usalama pamoja na kutoa taarifa ya mapato na matumizi ya kijiji hicho.

Alisema kuwa katika kijiji hicho kumekuwa na tabia ya muda mrefu kwa wafugaji kutembea wakimwa na sime, mkuki, mapanga na hata marungu hali inayosababisha hofu kwa baadhi ya wananchi kwani hawajui usalama wao wanapokutana na mtu huyo.

Mwenyekiti huyo wa ulinzi na usalama wa kijiji hicho alisema kuwa kutokana na kutembea na silaha hizo bila serikali yake kuchukua hatua baadhi yao wamekuwa wakiwapiga wananchi na hata kuwajeruhi hali ambayo haivumiliki kijijini hapo.

“ kuanzia leo hii ni marufuku kwa wafugaji kutembea na silaha za jadi kwakua hii inasababisha wawapige wananchi fimbo na kuwaumiza huku wengine wakienda katika sehemu za starehe kama harusini, mpirani wakiwa na fimbo na sime atakaye kamata atachukuliwa hatua”

Aidha aliliagiza jeshi la mgambo kijijini hapo kuhakikisha kuwa wanawasaka watakaokiuka amri hiyo ili kuondoa vitendo vya uvungaji sheria kwani hata migogoro ya wakulima na wafugaji inatokana na wengine kutembea na silaha hali inayosababisha kundi jingine litumie silaha yanapokabiriana makundi haya mawili.

Kufuatia marufuki hiyo baadhi ya wakazi wa kijiji hicho wakizungumza na gazeti hili waliushukuru uongozi wa kijiji hicho walidai kuwa tabia hiyo imekuwa ikiwakera kwa muda mrefu lakini walikuwa hawana namna ya kufanya.

Monica Kavishe mkazi wa kijiji hicho alisema kuwa baadhi ya wafugaji hao wamekuwa wakiwachapa fimbo na kuwajeruhi na wamekuwa wakifanya ubabe kijijini hapo kwa madai kuwa wanauwezo hata wa kifedha wa kuwadhibiti viongozi wa serikali lakini kutokana na maamuzi ya mwenyekiti Kanjele inaonesha ameamua kwenda na kasi ya serikali ya awamu ya tano ya rais John Magufuli.

Mwisho

No comments:

Post a Comment