Thursday 26 November 2015

Polisi Katavi wanasa Jangili


JESHI la polisi mkoani Katavi limefanikiwa kumnasa jangilii anayefahamika kwa jina la Xsavery Sikazwe(43) mkazi wa kijiji cha Igongwe kata ya Sitalike Tarafa ya Nsimbo Wilaya ya Mlele Mkoani humo ambaye alikuwa akisakwa kwa muda mrefu.
Kamanda wa polisi mkoani humo Dhahiri Kadavashari alisema kuwa kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo kunatokana na ushirikiano mwema uliopo baina ya polisi na wananchi ambapo polisi walipata taarifa za siri zilizosababisha kukamatwa kwa jangili huyo.
siku ya kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo polisi waliandaa mtego nyumbani kwa mtuhumiwa huyo ambapo polisi walijificha porini karibu na nyumba ya mtuhumiwa na ilipofika majira ya saa 12;30 za jioni walimuona mtuhumiwa akirejea nyumbani kwake ndipo walipomvamia na kumtia mbaroni.
Baada ya kumkamata walianza kufanya msako katika nyumba yake na hawakufanikiwa kupata kitu ndipo baada ya kumbana mtuhumiwa huyo aliwapeleka umbali wa mita tano kutoka katika nyumba yake na kuwaonesha polisi eneo ambalo walianza kufukua na kukuta mfuko wa sandarusi ambao ndani yake kulikuwa na jino moja la tembo pamoja na mikia miwili ya mnyama huyo.
Kamanda Kidavashari alisema kuwa kutokana na kupatikana kwa mikia hiyo miwili kunaonesha kuwa mtuhumiwa huyo aliua tembo wawili ambao wanathamani ya shilingi milioni 60 ambapo anashikiliwa na polisi.
Katika tukio jingine Kamanda huyo wa polisi alisema kuwa watu watatu waliofahamika kwa majina ya Juma Kapongo(55), Amos Kapongo(20) pamoja na Haruna Sikazwe(20) mkazi wa Sitalike wilayani Mlele walikamatwa wakiwa na silaha moja aina ya gobore ikiwa na risasi yake moja.

Kidavashari alisema kuwa watu hao walikamatwa kutokana na msako unaoendelea mkoani humo wenye lengo la kukomesha ujangili unaofanyika katika ifadhi ya taifa ya Katavi na mapori yake ya akiba kwani polisi ikishirikiana na kikosi cha askari wa wanyama pori wamedhamiria kuumaliza ujangiri katika hifadhi hiyo.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment