Thursday 26 November 2015

Acheni ujenzi holela.


HALMASHAURI ya Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa imewataka wakazi wa mji kusitisha ujenzi holela unaofanywa na wakazi hao ili kujiepusha na hasara wanazoweza kuzipata pindi watakapo bomolewa nyumba zao kutokana na kukiuka taratibu za mipango miji.

Ushauri huo umetolewa na mkurugenzi wa halmashauri hiyo Hamidu Njovu wakati akizungumza na gazeti hili lililotaka kujua mikakati  inayofanywa na halmashauri katika kukabiliana na tatizo la ujenzi holela unaofanywa na wakazi wa halmashauri hiyo kwa madai kuwa manispaa imeshindwa kuwapimia viwanja.

Alisema kuwa wakazi hao wanapaswa kufuata taratibu za mipango miji ili kuepuka kupata hasara itakapobidi kuwabomolea nyumba zao kwani baadhi yao wanajenga bila kufuata taratibu kitu ambacho ni hatari kwao na mali zao.

Mkurugenzi huyo alisema halmashauri hiyo imetenga maeneo ya viwanda na makazi ya watu lakini kitu cha kushangaza baadhi ya watu wamekuwa wakiyavamia maeneo hiyo na kujenga makazi ya kudumu kanakwamba hawajui kuwa hilo ni eneo la viwanda.

Alisema itakapofika wakati Manispaa inahitaji eneo lake kwaajili ya kuliendeleza italazimika kuwaondoa watu hao na wataanza kuilalamikia serikali wakati wao ndio walioenda kuvamia maeneo hayo huku wakijua sababu za kutengwa kwa eneo husika.

Kwaupande wake Frorian  Simbeye mkazi wa Sumbawanga mjini alisema kuwa yeye binafsi anashangazwa na agizo hilo la manispaa huku halmashauri hiyo ndiyo yenye wajibu ya kupima viwanja lakini haijafanya kazi hiyo kwa miaka mingi sasa kitu kinachosababisha wananchi wajenge kiholela.

Alisema ni lazima mkurugenzi ahakikishe anapima viwanja kila wakati na kwa wakati muafaka ili wananchi wajenge makazi yao lakini kuwalaumu kuwa wanafanya ujenzi holela wakati ofisi yake haijapima maeneo ni kutowatendea haki wananchi hao.

GURIAN  ADOLF

No comments:

Post a Comment