Thursday 26 November 2015

Acheni siasa chapeni kazi-DED

Na Gurian  Adolf





ILIYOKUWA tume ya uchaguzi jimbo la Sumbawanga mkoani Rukwa imewataka wakazi wa jimbo hilo kuachana na masuala ya siasa badala yake wajikite katika kufanya shughuli za maendeleo ambazo zitawaletea maendeleo katika maisha yao.

Mkurugenzi wa mji wa Sumbawanga Hamidu Njovu aliyasema hayo jana wakati akizungumza katika moja ya kituo cha redio kilichopo jimboni humo ambapo alikuwa akiwashukuru wananchi kwa kushiriki vizuri katika uchaguzi mkuu uliopita.

Alisema kuwa wakati wa siasa umepita na aliyeibuka na ushindi ni Aesh Hilary aliyefanikiwa kuitetea nafasi hiyo, hivyo basi hapana budi kwa wakazi wa jimbo hilo kuhakikisha wanamuunga mkono ili aweze kutekeleza majukumu yake na kuwaletea maendeleo.

Njovu alisema wakati wa kampeni watu waligawanyika katika makundi kufuatana na vyama vyao vya siasa lakini hivi sasa wakazi wa Sumbawanga mjini wanapaswa kuwa kitu kimoja na kukabiriana na maadui wakuu ambao mmoja kati yao ni umasikini.

Alisema itakuwa ni jambo la ajabu kuona baadhi ya watu wakiendelea na tofauti zao ambazo zilijitokeza katika uchaguzi mkuu kwa misingi ya itikadi za kisiasa kwani tayari wakati huo umepita na halmashauri imepata madiwani na mbunge ambao sasa wanawajibu wa kuwatumikia wananchi.

Naye Vanny Kansapa mkazi jimbo hilo alisema kuwa kinachosubiriwa hivi sasa ni kwa Hilary kuhakikisha anatekeleza ahadi alizoahidi wakati wa kampeni kwani wananchi walimpa kura wakiwa na imani naye kutokana na rekodi yake ya kuwatumikia.

Alisema kuwa moja ya changamoto zinazowakabiri wakazi wa mji huo ni tatizo la maji na kupitia mradi mkubwa unaotekelezwa na serikali ungeweza kumaliza kero hiyo lakini tatizo linaloonekana ni usimamizi mbovu ambao unasababisha mradi huo kutokamilika licha ya kuwa uko nje ya muda wake wa kukamilika kwa miaka miwili sasa huku wananchi wakiendelea kuteseka.

mwisho.

No comments:

Post a Comment