Tuesday 24 November 2015

DED SUMBAWANGA APIGA MKWARA

Na Gurian  Adolf

Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa Hamidu Njovu amewaonya baadhi ya wakazi wa manispaa hiyo kuacha tabia ya kupuuza sheria ndogo zinazotungwa na halmashauri hiyo kwani ipo siku tabia hiyo itawatokea puani.

Akizungumza na gazeti hili mkurugenzi huyo alisema kuwa wapo baadhi ya watu kwa makusudi wakijua kuwa kunabaadhi ya vitu vinakatazwa na sheria ndogo za manispaa hiyo lakini wanakiuka makusudi bila hofu ya kuchukuliwa hatua.

Akitolea mfano amesema kuwa moja ya sheria hizo ni suala la usafi kwa kila mkazi wa manispaa hiyo lakini wapo baadhi ya watu wamekuwa na tabia ya kutapisha vyoo,kufanya biashara katika mazingira machafu bila kuwa na hofu ya sheria pamoja usalama wa afya zao.

Mkurugenzi huyo wa Manispaa amesema kuwa tayari ametoa maagizo kwa watendaji wa halmashauri hiyo kusimamia suala la usafi ili kuepukana na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu kwani jitihada zisipofanyika ugonjwa huo unaweza kulipuka katika manispaa hiyo.

Aidha Njovu aliwataka vijana katika msimu huu wa kilimo kujishughulisha ili nyakati za mavuno weweze kupata mazao mengi ambayo yatawasaidia kupiga hatua katika maisha yao na familia zao.

Alisema vijana wanapaswa kutambua kuwa kunasheria ya nguvu kazi ambayo sasa imefika wakati lazima isimamiwe ipasavyo kwani wapo vijana wanaoshinda kijiweni bila kuzalisha huku wakiona mvua zinaendelea kunyesha na wao wamekuwa wakwanza kulia ugumu wa maisha.

Ameongeza kuwa huu ni wakati wa kutekeleza kaulimbiu ya Rais John Magufuli ya 'Hapa kazi tu" hivyo vijana hawanabudi kubadirika na kufanya kazi kwa bidii tofauti na hivyo watabaki wakililia ugumu wa maisha siku zote.

mwisho.

No comments:

Post a Comment