Tuesday 24 November 2015

INYONGA KUMUONA RAIS MAGUFULI

 Gurian   Adolf

WAKAZI wa kijiji cha Inyonga wilaya ya mlele mkoani Katavi wamedai kuwa wanafunga safari na kwenda Ikulu kwa lengo la kumuona Rais  John Magufuli ili kumueleza kuchoshwa na umasikini ambao serikali imewasasabisha kutokana na kushindwa kuwalipa fedha za fidia.

Walimueleza hayo mkuu wa wilaya hiyo Said  Njiku wakidai kuwa wamesubiri kwa takribani miaka minne sasa bila mafanikio licha ya kwamba walihakikishiwa wangelipwa fedha hiyo ndani ya muda mfupi.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake Fransi Jerememia alisema kuwa wakati wilaya hiyo inaanzishwa wakazi hao waliombwa watoe eneo la ardhi ambalo walikuwa wakiishi,kulima na kufuga ili serikali ijenge hospitali ya wilaya kwa makubaliano ya kulipwa fidia lakini suala hilo limekuwa ni adhabu kwao.

Alisema kuwa baada ya kukubali ombi hilo la serikali waliambiwa waache kufanya ujenzi,kilimo,ufugaji na shughuli nyingine kwani watapewa fidia ili wakatafute maeneo mengine lakini hali imekuwa ni tofauti mpaka sasa wanaishi maisha ya dhiki kutokana na kutokuwa na ardhi.

‘’tulitegemea tungelipwa fidia ndipo tungeenda kununua ardhi ili tujenge na kuendelea na maisha yetu huko lakini mpaka sasa hakuna kinachoeleweka kwa hivyo tumechoka sasa ni kwenda kumuona rais tu ndiyo tunaamini atatusaidia serikali ya wilaya imeshindwa kabisa’’….alisema.

Naye Maria Simwanza mkazi wa kijiji hicho alisema kuwa mpaka sasa wamekwisha changishana fedha kiasi cha shilingi 800,000  fedha ambazo zitatumika kama naauri na kujikimu watu ambao watakwenda kumuona raisi kwani wanaishi maisha ya dhiki huku wakisikitika kuwa serikali ndiyo inayowatesa kwa kiwango hicho.

Alisema pamoja na kuwa mkuu wao wa wilaya ameahidi atalishughulikia suala hilo wamedai kuwa kila mara amekuwa akiwapa majibu ya kisiasa ambayo pia wameyachoka iliyobaki ni kumuona raisi tu huenda yeye atapatia ufumbuzi suala hilo kwani wanazidi kuwa masikini wa kutupa kutokana na kutokuwa na ardhi.

Hata hivyo mkuu huyo wa wilaya ya Mlele Said Njiku aliwasihi wananchi hao kuwa wavumilivu pamoja na changamoto hizo lakini wanapaswa kutambua kuwa serikali itawalipa na tatizo hilo litakwisha kabisa.

mwisho  


No comments:

Post a Comment