Wednesday, 3 June 2015

Mchungaji Mbaroni kwa ubakaji.

Na Gurian  Adolf
Sumbawanga.


MCHUNGAJI wa kanisa  la Evangelical Assemblies Of God Tanzania ( EAGT )  kijiji cha  Ntuchi kata ya Isale wilayani Nkasi mkoani Rukwa Evans Kankoma (41) anatuhumiwa kumbaka mtoto wa miaka 5 ambaye ni mwanafunzi wa darasa la awali katika shule ya  msingi ya Ntuchi.


Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana na kuthibitishwa na afisa mtendaji wa kijiji hicho Robert  lunyelele  ni kuwa mtoto huyo alibakwa majira ya saa 7 mchana kwenye bustani ya miti pamoja na matunda  ambapo mtoto huyo akiwa na mwenzie wametoka shule walipitia kwenye bustani hiyo  kwa lengo la kwenda kuchuma mapera.


Mchungaji huyo alimwita mtoto huyo huku akimlazimisha mwanafunzi mwenzie aliyekua naye kwenda nyumbani na ndipo alipoanza kumbaka  mtoto huyo ambaye alipata maumivu makali.


Afisa mtendaji huyo wa kijiji alifafanua kuwa chanzo cha kuibuliwa kwa jambo hilo lilitokana na Yule mwanafunzi mwenzie aliyeambiwa aende nyumbani ndiye aliyetoa taarifa na ndipo wazazi walipoamua kufuatilia kwenye bustani hiyo na kumkuta mchungaji eneo hilo huku mtoto huyo akilia  kutokana na maumivu makali aliyoyapata.


Alisema  baada ya hapo wazazi wa mtoto huyo walipiga kelele zilizowezesha watu kufurika eneo hilo na kujionea tukio hilo na ndipo walipomkamata na kumfikisha mbele ya serikali ya kijiji hicho.


Kwa upande wake afisa mtendaji wa kata ya Isale Deogratius Selemani  alikiri kutokea kwa tukio hilo na kuwa wakati tukio hilo likitendeka  yeye alikua kwenye ofisi ya afisa mtendaji wa kijiji  hicho na kuwa wazazi  wa mtoto huyo walitaka kufikia makubaliano ya kulimaliza jambo hilo katika ofisi hiyo ya kijiji  kwa mchungaji huyo kulipa faini na ndipo yeye kama mtendaji wa kata  alikataa  na kumtaka mtendaji wa kijiji kulilipoti tukio hilo polisi.


Alisema baada ya polisi kupata taarifa hizo walifika mara moja eneo la tukio na kumkamata mtuhumiwa huyo kwa ajiri ya taratibu nyingine za kisheria.


Awali  viongozi waandamizi wa kanisa hilo ambao hawakupenda majina yao kutajwa  katika gazeti hili walidai kuwa tukio hilo wao limewafedhehesha sana na kuonekana kana kwamba na wao wana tabia kama hizo za mchungaji wao na kuwa kanisa sasa limezorota baada ya waumini kumeguka vipande vipande.


Walisema kuwa wao kama waumini wa kanisa hilo na viongozi ule ujasiri waliokuwa nao awali wa kupita mbele ya watu kuwa wanamjua  Mungu hivi sasa ujasiri huo haupo na hawaonekani mbele za watu kwa sasa kuikwepa aibu hiyo.


Mchungaji huyo kwa sasa anashikiliwa na jeshi  la polisi na taratibu za kiupelelezi zikikamilika atafikishwa mahakani wakati wowote kuanzia sasa.


mwisho


No comments:

Post a Comment