KATIBU MKUU WA CCM NDUGU KINANA KUANZA ZIARA KESHO KUELEKEA KAGERA, GEITA ,MWANZA
Katibu wa NEC-CCM Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye akizungumza
mapema leo jijini Dar na Waandishi wa habari, alieleza kuwa wataondoka jijini Dar kesho kwa basi
maalumu, ambapo watasimama njiani katika mikoa ya Morogoro, Dodoma,
Singida na mengineyo kwa ajili ya kusalimia wananchi.
Katibu wa NEC-CCM Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye akisisitiza jambo zaidi kwa Waandishi wa habari, kuhusiana na ziara hiyo itakayoanza kesho.
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana anatarajia kuanza ziara ya siku 28 kesho katika mikoa mitatu ya Kagera, Geita na Mwanza kukamilisha mikoa yote 30 nchi nzima.
Ziara hizo zenye malengo ya kukagua utekelezwaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM mwaka 2010 na kuimarisha chama zimekuwa na mafanikio kwa kuondoa matatizo mbalimbali yanayowakumba wananchi hasa wa mikoani.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar leo, Katibu wa NEC-CCM Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alisema wataondoka jijini Dar kesho asubuhi kwa basi maalumu, ambapo watasimama njiani katika mikoa ya Morogoro, Dodoma, Singida na mengineyo kwa ajili ya kusalimia wananchi.
“Ziara rasmi itaanza June 4 katika Wilaya ya Nyakanazi mkoani Kagera, lakini kesho tutakunywa chai Morogoro chakula cha mchana tutakula Dodoma halafu tutasalimia wananchi katika Mikoa ya njiani kama Singida, Nzega na tumepanga kulala Kahama mkoani Shinyanga, tukiamka ziara ndio itaanza rasmi,” alisema Nape.
Aliongeza kuwa katika ziara hiyo watatembelea majimbo yote ya uchaguzi hivyo amewataka wana-CCM na wananchi wengine kujitokeza kwa wingi kumsikiliza Katibu Mkuu katika ziara hiyo ya kihistoria.
“Hii ni ziara ya kihistoria kwa sababu ya mambo matatu, kwanza tutatembelea visiwa vyote vya Ukerewe ambavyo ni nadra kutembelewa na viongozi, pili huu ni mwaka wa uchaguzi kuna masuala mengi yanahitaji ufafanuzi,” alisema.
Akitaja ratiba ya ziara hiyo Nape alifafanua kuwa, “Kuanzia Juni 5 mpaka Juni 15 tutakuwa Mkoa wa Kagera, Juni 16 mpaka 21 tutakuwa Mkoa wa Geita na Juni 22 mapaka Julai 2 tutakuwa Mwanza kuhitimisha ziara ya nchi nzima kwa mkutano mkubwa wa kihistoria.”
Akijibu maswali ya waandishi wa habari kuhusu faida za ziara hizi Nape alisema kuna masuala mengi ya kimaendeleo yalisimama lakini alipopita Katibu Mkuu Kinana ufumbuzi umepaikana, akitolea mfano mashamba yaliyobinafsishwa bila kufuata utaratibu alisema Rais Jakaya Kikwete, amefuta hati nyingi za mashamba ya wawekezaji na kurudishwa kwa wananchi.
“Kuna baadhi ya maeneo kulikuwa na zahanati zimeshajengwa lakini hakuna vibali, nimepata taarifa kuwa vibali vimeshapatikana na huduma zinaendelea, kulikuwa na matatizo ya ardhi za wananchi kuchukuliwa na wawekezaji katika maeneo ya Tanga, Arusha, Babati na maeneo mengine lakini kila kitu kipo sawa sasa na wananchi wanamshukuru Kinana,” alisema.
Aliongeza kuwa, “Nisisitize kuwa tumesema tutaondoka na basi maalumu kwa sababu kama kuna mwingine atafanya hivyo atakuwa ametuiga, mkumbuke hili wazo la kuondoka na basi ni la Katibu Mkuu.”.
Ikiwa ziara hizi zitamalizika salama Julai 2 mwaka huu, Kinana atakuwa Katibu Mkuu pekee wa CCM tangu kuanzishwa kwake Februari 5, 1977 kuzunguka nchi nzima kuangalia uhai wa chama na kusikiliza na kutatua kero za wananchi wote bila kujali itikadi za vyama.
No comments:
Post a Comment