Na Walter Mguluchuma
Katavi
Mkuu wa wilaya ya Mpanda mkoani Katavi Lilian Matinga ameitaka halmashauri ya wilaya ya Nsimbo kuhakikisha inawalipa madeni wazabuni ifikapo Machi 31 na endapo ikishindwa kuwalipa isikope tena kwa wazabuni hao mpaka itakapo maliza kuwalipa.
Mkuu huyo wa Wilaya ya Mpanda alitoa agizo hilo juzi wakati wa kikao cha baraza la biashara la Mkoa wa Katavi TCCIA kilichofanyika katika ukumbi wa idara ya maji mjini hapa .
Matinga alisema kuwa halmashauri ya hiyo ndio inayoongoza katika Halmashauri zote tano zilizopo katika Mkoa huo kwa kuwa na madeni mengi wanayodaiwa na wazabuni mbalimbali ambao wametoa huduma kwenye halmashauri hiyo kwa kipindi cha muda mrefu sasa.
Alisma kuwa yeye kama Mkuu wa Wilaya amekuwa hafurahishwi na tabia ya halmashauri hiyo kushindwa ya kuwalipa wazabuni wake na huku bado wakiendelea kukopa madeni mengine kwa wazabuni hao.
Alisema ni jambo la kusikitisha sana kwa halmashauri kushindwa kulipa hata mzabuni wa chakula hivyo alimwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Nsimbo kuhakikisha ifikapo Machi 31 kulipa madeni yote wanayodaiwa na wazabuni wao wawe wameyalipa vinginevyo waache kabisa kukopa kwa wabuni mpaka hapo watakapo kuwa wamelipa.
Miongoni mwa wazabuni wanayoidai Halmashauri ya Nsimbo toka mwaka 2012 ni wazabuni wa chakula ,stationary na wakandarasi wa majengo mbalimbali.
Naye Mwenyekiti wa TCCIA wa Mkoa wa Katavi Hassanal Dalla alisema madai ya wazabuni hao yamekuwa ni ya muda mrefu sasa na yamesababisha baadhi ya wafanya biashara kushindwa kuendeleza shughuli zao na baadhi yao kufilisika kabisa .
Alisema wazabuni wamepata usumbufu mkubwa kutoka kwenye taasisi mbaimbali za kibenki ambako wafanyabiashara hao walichukuwa mikopo na wameshindwa kurudisha kwa wakati kwani wanadaiwa mara kwa mara.
Kwa upande wake Amani Mahera mwenyekiti wa jumuia ya Wafanyabiashara Tanzania tawi la Mkoa wa Katavi alisema kuwa hari hiyo ya kutolipwa kwa wazabuni madai yao kumewasababishia baadhi yao kufunga biashara zao na wengine kufilisika .
Hivyo aliiomba halmashauri hiyo kuwalipa fedha zao wazabuni hao ili nao waweze kulipa kodi za serikali kwani inashangaza kwa mfanyabiashara kufungiwa kampuni na biashara zake na mamlaka ya kukusanya mapato kwa kosa la kushindwa kulipa kodi wakati nayeye fedha zake zipo anaidai halmashauri.
Mwisho
No comments:
Post a Comment