Monday 1 January 2018

Washikiliwa na takukuru kwa kupokea rushwa kwanjia ya simu

Na Gurian Adolf
Nkasi
WATUMISHI Wanne wa idara ya ardhi na maliasili wilayani Nkasi mkoani Rukwa wanashikiliwa na taasisi ya kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa kosa la kuomba na kupokea rushwa ya Tshs,1,200,000  kutoka kwa Wafugaji.
Kwamujibu wa taarifa iliyotolewa kwa waandishi wa habari na mkuu wa wilaya,Said Mtanda mbele ya wakuu wa idara wa halmashauri hiyo alisema kuwa Watumishi hao walikamatwa juzi majira ya saa 2 usiku baada ya kutegewa mtego.
Alisema kuwa siku moja kabla ya kukamatwa kwa watumishi hao walifanya operesheni ya kukamata mifugo inayochungwa ndani ya hifadhi ya msitu wa Mfili na kufanikiwa kukamata ng’ombe 40 waliokuwa wameingia katika hifadhi hiyo kinyume cha sheria na kuwalipisha kuwatoza wafugaji faini ambapo walitoa fedha taslimu shilingi 350,000 huku wakiwataka fedha nyingine kiasi cha shilingi 850,000 wazilipe kupitia M-Pesa kwakua kwakua walikua hawana wakati huo.
Alisema kuwa ofisi yake ilipata taarifa hizo na kuamua kuweka mtego kwa kuwashirikisha maafisa wa TAKUKURU na hatimaye waliweza kuzinasa fedha hizo zilizokuwa zimetumwa kupitia Akauti hiyo ya M-Pesa.
Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa maafisa hao walifanya kitendo hicho kinyume cha sheria na bila ya kutoa risiti ambapo wakati wa zoezi la kutoa fedha hizo walimtumia mke wa mmoja wa maafisa hao kwenda kutoa fedha hizo ambapo naye anashikiliwa na taasisi hiyo ya kuzuia rushwa.
Aliwataja watumishi hao ambao bado wanashikiliwa kuwa ni Nicodemus Hillu afisa ardhi na maliasili,na askari wanyapori ambao ni Sylivesta Soneka,Justin Makandi,Anselimo Godian pamoja na mke wa mmoja wa maofisa hao Rahel Nkumbo ambaye alitumika kama wakala katika zoezi hilo la kukamilisha njama hizo za rushwa.
Aliwataka watendaji wa serikali kuwa makini hasa katika kipindi hiki cha serikali ya awamu ya tano kwa kuhakikisha kuwa wanafanya kazi zao kwa kuzingatia kanuni na kwa kufuata maadili ya utumishi wa Umma na kuwa serikali hivi sasa haipo tayari  kuwavumilia watumishi ambao ni watovu wanidhamu. 
Kwaupande wake mbunge wa jimbo la Nkasi Kasikazini Ally Kessy  alisema kuwa katika kipindi hiki ambacho serikali inapambana na vitendo vya rushwa na ufisadi  bado wapo baadhi ya watumishi ambao hawataki kubadilika na kuwa watu wa namna hiyo wachukuliwe hatua  kwani hayupo tayari kuwasaidia watumishi wa namna hiyo.
Alisema kwa kuwa bado kuna watu ambao hawataki kubadilika na kuenenda sawa na serikali ya awamu ya tano watahakikisha watumishi hao wanashugulikiwa  ili iwe ni mfano kwa wengine ambao wana tabia kama hizo.
Katibu tawala wa  wilaya  Festo Chonya alisema kuwa serikali ilishatoa dira ya nini kifanyike na katika mapambano ya rushwa katika serikali hii ya awamu ya tano na kutaka kila mmoja afanye kazi zake kisheria na kwa kutoa huduma kwa jamii na kuwa hakuna atakaeonewa huruma kama atakwenda kinyume cha sheria
Afisa utumishi wa halmashauri Asubisye Rajae alisema kuwa idara yake ndiyo inayoshughulika na nidhamu kwa Watumishi na kuwa watahakikisha watumishi hao wanashughulikiwa kinidhamu licha ya kuwa taratibu nyingine za kisheria zitakuwa zikichukuliwa na kutoa rai kwa watumishi  kuhakikisha kuwa maadili yanazingatiwa katika utendaji wa kazi  za serikali.
Mwisho

No comments:

Post a Comment