Sunday, 10 December 2017

Jela miaka 20 kwa kukatwa na nyama ya kiboko

Na walter Mguluchuma
Katavi
Mahakama ya wilaya ya  Mpanda mkoani  Katavi imemuhukumu  Omary  Maganga(45) kwenda jela miaka 20 baada ya kupatikana na  hatia ya kukamatwa na nyama ya Kiboko zaidi ya kilo 100.
Akisoma hukumu hiyo hakimu  mkazi  mfawidhi wa  mahakama ya  wilaya ya  Mpanda  Chiganga  Ntengwa  alisema mahakama  imeridhishwa na  ushahidi uliotolewa  na upande wa  mashitaka ukiongozwa na wanasheria wa  Serikali Fraviani Shio.
Awali  katika  kesi  hiyo mwendesha  mashitaka mwanasheria wa  Serikali   Shio aliieleza mahakama hiyo kuwa Maganga ambaye ni mkazi wa Kijiji cha  Itenka  Rarafa ya  Nsimbo, alitenda  kosa  hilo oktoba 10 mwaka 2016 majira ya  saa 11 za jioni.
 Alieleza  kuwa  siku ya tukio  mshitakiwa  alikamatwa   akiwa  ndani ya  Hifadhi ya  Taifa ya  Katavi  huku  akiwa  na  nyama ya  kiboko  yenye uzito wa kilo 118 yenye  thamani ya shilingi milioni  3,274,500.
Mwanasheria   huyo aliiambia  mahakama kuwa  mshitakiwa  huyo  alikamatwa  na  askari wa   Hifadhi ya  Taifa ya  Katavi  baada  ya kupata taarifa kutoka kwa raia  wema za kuwa   mshitakiwa amekuwa akifanya ujangili kwenye hifadhi ya Taifa na  ndipo walipoanza msako na kufanikiwa kumkamata  siku  hiyo akiwa ndani ya Hifadhi ya Katavi huku akiwa na nyama hiyo ya Kiboko.
Akisoma  hukumu  hiyo  hakimu Ntengwa alisema kuwa  kutokana  na  ushahidi uliotolewa  mahakamani  na  upande wa  mashitaka ambao  ulikuwa  na  mashahidi watano na mshitakiwa  hakuwa  na  shahidi yeyote alisema   Mahakama  pasipo shaka yoyote imemkuta na hatia  mshitakiwa na kwakupitia kifungu cha sheria  namba  86 kifungu   kidogo cha  kwanza na cha pili  cha sheria ya  wanyama  pori namba 5 ya  mwaka 2009 imemtia hatiani.
Hivyo kabla ya  kusoma  hukumu  alitoa  nafasi kwa  mshitakiwa kujitetea na  kama pia anayosababu yoyote ya  msingi ya kuweza kuishawishi  Mahakama  iweze kumpunguzia  adhabu.
Mshitakiwa  katika  utetezi wake aliiomba  mahakama impunguzie  adhabu  kwa kwa  kile aichodai  hilo  lilikuwa ni kosa   lake  la  kwanza  katika  maisha yake  na  pia  anayofamilia   ambayo  inamtegemea ya  mke na watoto pamoja na wazazi wake .
Utetezi huo ulipingwa vikali na  mwanasheria wa  Serikali, Shio ambaye  aliiomba  Mahakama  itoe   adhabu kali kwa  mshitakiwa ili   iwefundisho kwa watu wengine  wenye  tabia ya kuhujumu uchumi wa nchi.
Hakimu  Ntengwa  baada ya  kuzisikiliza pande zote mbili  alisema  kutokana  na makosa yaliomtia  hatiani mtuhumiwa imemuhukumu kwenda  jela miaka 20 kuanzia  juzi  na  kama  haja ridhika   na  adhabu hiyo  anayo nafasi ya kukata rufaa kwenye  mahakama ya juu zaidi.

No comments:

Post a Comment