Sunday 1 October 2017

Wakulima wa tumbaku walalamika kutolipwa

Na Walter Mguluchuma
Katavi
WAKULIMA wa tumbaku mkoani katavi wamelalamikia kutolipwa fedha za mauzo ya tumbaku huku baadhi ya makampuni yanayonunua tumbaku mkoani humo yameshindwa kununua zao hilo kwamadai kuwa wakulima wamezalisha kuliko uwezo wanunuzi hao.
 Wakizungumza na gazeti  hili wakulima hao walisema kitendo hicho kimewakatisha tamaa ya kulima zao hilo  kwa  msimu  ujao ambao unapaswa  kuanza   mwezi Septemba kwa kuotesha mbegu za zao hilo ambalo nitegemeo kwa uchumi kwa wakazi wa Mkoa wa huo. 
Akizungumza na gazeti hili mmoja wa Wakulima wa tumbaku wa Chama cha msingi cha  ushirika wa  wakulima wa  tumbaku  Mpanda Kati  George  Ngamila  alisema  kuwa  toka walipo uza  tumbaku yao kupitia  chama  chao  cha  msingi  cha Mpanda  kati  mwanzoni mwa  mwezi  Mei mpaka  sasa  hawajalipwa fedha zao.
Alisema kuwa  msimu wa  kusia mbegu za tumbaku  umeanza tangu mwezi septemba na  utamalizika  mwezi oktoba  lakini wakulima  wengi wameshindwa kusia  mbegu kutokana  na  kutolipwa  fedha zao za msimu iliopita huku  tumbaku  nyingine  ikiwa imerundikana kwenye  maghala ya kuuzia tumbaku na  nyingine kwenye nyumba za wakulima hao.
Ngamila alisems kuwa  wamekuwa wakipewa  taarifa na viongozi wao wa  chama cha  ushirika  cha  Mpanda  Kati kuwa  kuna kilo zaidi ya laki tano hazija nunuliwa  na  Kampuni  ya PREMIUM  kutokana na kuzidi kwa uzalishaji wa zao hilo katika  msimu uliopita.
Naye  Cretus Kagoma  mwanachama wa Chama cha msiingi  cha  Ushirika cha wakulima wa tumbaku  cha  Katumba  alisema kutokana na kutolipwa  malipo yao hadi sasa zaidi ya kilo  laki nne  baadhi ya  wakulima  wanakabiliwa na ugumu wa  maisha.
 Aliseama  kutoka na kutolipwa  fedha zao na wengine kutonunuliwa  tumbaku yao na  Kampuni ya ununuzi  ya  TLTC  kwa  kile  kinachodaiwa uzalishaji  umezidi  malengo waliokubaliana    baina ya   chama   chao cha ushirika  na   Kampuni ya  TLTC  wamepoteza  kabisa  matumaini ya  kulima tena  Katika msimu ujao.
Alisema kuwa  baadhi ya wakulima walikuwa wameingia mkataba  na  vibarua kuwafanyia  shughuli za  kilimo hivyo  wanaendelea  kuwahudumia  kwa chakula hadi  sasa  wakati  wakiwa  wanasubilia  kulipwa  malipo yao.
Kwaupande wake meneja wa  Chama cha msingi   Mpanda  Kati Amani  Rajabu  alieleza  kuwa  tatizo la  tumbaku  ya baadhi ya wakulima imesababishwa  na wakulima  wenyewe kulima  zaidi ya  makisio  yao  hali ambayo  imesababisha   kampuni  inayonunua  tumbaku  kushindwa kununua  tumbaku ya ziada. 
Akizungumzia suala la malipo ya  mauzo yao ya Tumbaku  Meneja  huyo  alisema  kuwa  wakulima   wenyewe waliamua  kwenye mkutano wao  mkuu kuwa malipo yatakuwa yanafanyika baada ya  masoko yote kuwa  yamemalizika  hivyo kwenye  chama hicho  bado  kuna kilo zaidi ya  laki tano ambazo hazija nunuliwa baada ya kuwa zimezidi kwenye  makisio yao ya msimu wa kilimo wa  mwaka 2016 /2017.
Amani  alisema  hata  hivyo baadhi ya wakulima walisha  peleka   malalamiko yao kwa  Mkuu wa  Mkoa huo ambaye  aliunda  tume ya kuchunguza  sababu  iliofanya kuwepo kwa  ongezeko la ziada la uzalishaji wa zao hilo  tofauti na  mika iliyopita.
Msimu wa ununuzi wa zao hilo ulianza  mwezi mei mwaka huu  na ulisimama  kuanzia  mwezi   septemba  baada ya  kampuni  yanayonunua   tumbaku kusitisha kununua baada ya kilo walizokuwa wamewekeana  mikataba na  vyama vya ushirika kuwa  zimefikia idadi .
Changamoto ya ongezeko la kilo za  tumbaku  limetokea katika  vyama  vyote vya   msingi  vya  ushirika mkoani  humo na  kusababisha  baadhi ya  wakulima  kushutumiana  kuwa  tumbaku  nyingi iliyouzwa sio ya wakulima  bali ni ya walanguzi kutoka mikoa ya jirani na kuiuzia  mkoani Katavi .
Mwisho

No comments:

Post a Comment