Sunday 8 October 2017

Albino kuwekewa ulinzi


Na Gurian Adolf

Sumbawanga
Muungano wa asasi zisizo za Kiserikali katika Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa, (SUMANGO) umeanza mchakato wa uundaji wa mabaraza ya kata lengo likiwa ni kuwalinda watu wenye ulemavu wa ngozi (Albinism) dhidi ya watu wenye nia mbaya ambao wamekuwa wakitishia maisha yao kwa kuwajeruhi kwa kuwakata viungo vya miili yao na kutoweka navyo.

Mratibu wa Asasi ya Sumango iliyopo mjini humo, Vincent Kuligi alisema hayo jana wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara uliolenga kutoa mafunzo kwa wananchi wa kata ya Malangali kabla ya kuunda mabaraza hayo, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa kuwalinda watu wenye ulemavu wa ngozi unaotekelezwa na asasi hiyo kwa ufadhili wa shirika lisilo la kiserikali la Foundation for Civili Society.  

Kuligi alisema kuwa uundaji wa mabaraza ya kata utasaidia  kuwalinda watu wenye ulemavu dhidi ya watu wenye nia mbaya ambao mara nyingi wamekuwa wakiwajeruhi kwa kuwakata viungo vyao na kuvipeleka kwa waganga wa jadi wakiwa na imani potofu kuwa watapata utajiri ama mafanikio ya kimaisha.

"Jukumu la kuwalinda walemavu wa ngozi tunalirudisha kwa jamii yenyewe kwa kuunda mabaraza ya kata, ambayo sasa yatakuwa na wajumbe wapatao 30 ambao watatoka ngazi za mitaa na watakuwa walinzi wa Albinism pindi inatokea kuna mtu au kikundi cha watu kinataka kuwadhuru na watatoa taarifa polisi ili hatua zichukuliwe haraka iwezekanavyo" alisema Kuligi.

Alisema kuwa walemavu wa ngozi ni sawa na watu wenye wengine hivyo wanapaswa kupata haki zote za msingi ikiwa pamoja na kuishi bila hofu yoyote ile, hivyo Sumango katika kutekeleza mradi huo wameona ni vema sasa wakaunda mabaraza hayo.

"Tunataka walemavu wa ngozi wapate haki zao zote kama kupata elimu, huduma za afya, washiriki katika kazi za kijamii...... kimsingi wasitengwe kwa namna yoyote ile" alisisitiza Kuligi.

Naye, Mtetezi wa Haki za Binadamu kutoka jijini Dar es Salaam, Maria Challe alisema kuwa umefika wakati  jamii inapaswa kubadilika kifikra na kuacha kuwaona albinism mitaji ya kuwapatia mafanikio ya kimaisha kupitia biashara na shughuli zao nyingine.

Maria ambaye pia ni mlemavu wa ngozi alisema  kuna dhana potofu iliyojenga miongoni mwa baadhi ya watu katika jamii kuwa ukikata kiungo cha albinism na kupeleka kwa maganga wa jadi utapata utajiri haipo ila kinachotakiwa ni kufanya kazi kwa bidii ndio siri ya mafanikio wala sio vinginevyo.  

Alisema pamoja na vyombo vya dola kuwa mstari wa mbele kuwalinda lakini bado jamii inapaswa kuelimishwa kuhusu umuhimu wa kuwalinda watu hao na kuhakikisha wanapata haki zao za msingi kama walivyo watu wengine.

Mwisho. 

No comments:

Post a Comment