Friday 21 July 2017

Wazazi Sumbawanga washauriwa kuwapa chakula bora watoto wao

Na Gurian Adolf
Sumbawanga
WAZAZI katika Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa wameshauliwa kuwapa chakula bora  watoto wao ili waweze kuondokana na tatizo la udumavu linalowakabiri watoto katika mji huo.
Akizungumza na Tabibu Dkt Godwin Kaswiza ambaye ni mganga wa kituo cha Afya cha Katandala mjini Sumbawanga alisema kuwa changamoto kubwa iliyopo kwa baadhi ya wazazi ni kutowajali watoto wao kwa kuwapa vyakula  vya aina tofauti ambavyo  vitawasaidia kukua  vizuri na kuondokana  na tatizo la  udumavu linalowakabiri watoto wengi katika mji huo.
Alisema kuwa wengi wa wazazi katika mji huo wanatumia fedha zao katika mavazi, kunywa pombe na starehe nyinginezo na kusahau kabisa kuwekeza katika vyakula  vya watoto wao ambao wanahitaji  kukua  vizuri na moja kati ya kigezo muhimu ni chakula bora.
Dkt Kaswiza alisema kuwa walau kila mzazi angejali kumpa  mtoto wake hata bilauli moja ya maziwa kila siku na mayai ya kuku walau matatu kwa wiki pamoja na kumpa  uji  unaotengenezwa kwa unga safi wa lishe  tatizo la  kudumaa kwa watoto lingepungua kwa kiasi kikubwa katika mji huo.
Alisema kuwa mpaka hivi sasa takwimu zinaonesha kuwa asilimia 70 ya watoto katika mkoa wa Rukwa wamedumaa lakini mkoa huo ni miongoni mwa mikoa inayozalisha chakula changamoto iliyopo ni elimu ya kula kwani wazazi wamekuwa wakifikiria zaidi kuuza chakula na kupata fedha bila kufikiri kuhusu chakula cha watoto wao.
Dkt huyo alisema kuwa imefika  wakati wataalamu wa lishe  katika mji huo kutoa  elimu ya kutosha ambapo kama jamii itapata  elimu ya kutosha itasaidia pia kukabiliana na baadhi ya magonjwa yanayohitaji lishe  nzuri kwani ndiyo yamekuwa  ni kikwazo cha maendeleo ya watoto wao ki mwili na kiakili. 
Alisema kuwa wanasiasa mjini humo wanapaswa kulipa kipaumbele suala la  lishe  kwa wapiga  kura wao kwani kama watawekeza katika lishe  bora watakua na afya nzuri na wataendelea  kuwapigia kura kwa muda mrefu na hata bajeti ya afya itapungua kwakua wananchi watakua na afya bora.
Naye mganga wa hospitali ya mkoa wa Rukwa Emmanuel Mtika akizungumza na gazeti la  Tabibu alisema kuwa ni vizuri watu wakafundishwa namna  ya kula vyakula  vitakavyowapa afya nzuri kwani hivi sasa kuna tatizo la  ulaji vyakula  visivyofaa kwa afya hali inayochangia kuongezeka kwa magonjwa ambayo yanatokana na ulaji vyakula  bila kufanya mazoezi na matokeo yake kujikuta wakipata tatizo la  unene  uliopitiliza.
Alisema kuwa vifo vingi hivi sasa vinatokana na magonjwa yasiyo ambukiza ambayo mengi yanatokana na utaratibu  mbaya wa kula vyakula  bila kufanya mazoezi na kupima afya na hii imekuwa  changamoto kubwa kwani tatizo hili linazidi kukua  siku hadi siku.
Mwisho

No comments:

Post a Comment