Friday 21 July 2017

Naibu waziri asikitishwa hospitali ya mkoa kukosa Damu

Na Gurian Adolf
Sumbawanga
Naibu Waziri wa Wizara ya Afya Dk Hamis Kigwangala amesikishwa na kitendo cha hospitali ya mkoa wa Rukwa kukosa damu ya kutosha kwaajili ya kuwasaidia wagonjwa pindi dharura inapotokea.
Masikitiko hayo aliyabainisha jana baada ya kufanya ukaguzi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa katika ziara yake ya siku moja katika mkoa huo ambapo alitembelea hospitali hiyo pamoja na vituo vya afya vitatu vya Laela Wilayani Sumbawanga, Wampembe na Nkomolo vya Wilaya ya Nkasi.
Dkt Kigwangala alisema kuwa hajafurahishwa na hali aliyo ikuta katika hospitali hiyo kwani inachangia  kuzorotesha lengo la  serikali katika kutoa  huduma za afya kwani moja kati ya mikakati ni kuhakikisha kuwa wagonjwa wanapata  huduma.
“Nimesikitishwa na changamoto ya upatikanaji wa damu, kwanza mna units chache mlipaswa kuwa na units karibu 120 ili kuendana na idadi ya watu milioni 1.2 wa mkoa mzima, lakini kwa bahati mbaya hamna hata damu moja ambayo imekuwa “screened” na tayari kwa matumizi, hii inasikitisha sana lakini kwa ujumla maabara iliyopo ni nzuri sana, kuna mapungufu machache sana kwenye “theatre” na pia nimefurahishwa na “labour ward” iko vizuri sana" alisema
Dk. Kigwangala alibainisha kuwa changamoto ya upatikanaji wa damu ipo katika kanda ya nyanda za juu kusini na kuahidi kulishughulikia jambo hilo huku akiwaasa wananchi kujitokeza kwa wingi kuchangia damu na si kukaa pembeni na kulalamika pindi wanapokosa damu hospitali wakati wanashindwa kujitolea damu.
“Mimi binafsi najitolea damu mara tatu kwa mwaka, wananchi tunatakiwa kujitolea damu ili kuweza kuwasaidia wale wanaohitaji, huwezi jua inaweza kumsaidia ndugu, jirani ama rafiki, hivyo tuwe na moyo wa kujitolea damu.” Alisema.
Katika ziara yake hiyo mambo aliyoyapa kipaumbele ni kuangalia huduma za maabara, vyumba vya upasuaji, vyumba vya kuzalia pamoja na akiba ya damu salama, ambapo vituo hivyo vilionekana kufanya vizuri katika maeneo hayo.
Huduma ya maji katika vituo hivyo ilioneka kuwa ni kikwazo katika upatikanaji wa huduma bora ambapo Dk. Kigwangala aliwaagiza wakurugenzi wa Sumbwanga Vijijini pamoja na Halmashauri ya Nkasi kuhakikisha jambo hilo linatafutiwa ufumbuzi wa haraka kwa kutambua umuhimu wa maji na ubora wa huduma za afya.
Dk. Kigwangala hakutaka ziara hiyo iwe ya kiutendaji pekee hivyo alikutana na wananchi wa maeneo ya Laela pamoja na Wampembe na kuwapa nafasi ya kueleza changamoto wanazokutana nazo katika kupata huduma bora za afya.
Ndipo alipojitokeza ndugu Nassoro Ibrahim na kutaka kufahamu nafasi ya walemavu katika kupata huduma bure kama ilivyo katika makundi ya wazee, watoto na wajawazito, “Naomba Serikali ituangalie na sisi walemavu tunnapata shida sana maana wenzetu wazee, watoto na kinamama wanasaidiwa,”Alisema.
Katika kujibu swali hilo Dk. Kigwangala alimtaka mlemavu huyo kuonana na uongozi ili aweze kufuata taratibu za kuweza kutibiwa bure lakini alimuahidi kuwa serikali ipo katika mkakati kuona namna ambayo wanaweza kuwasaidia walemavu katika kupata huduma bure.
Mwisho

No comments:

Post a Comment