Wednesday 19 July 2017

Wanao tetea wanafunzi waliojifungua kurudi shule waonywa

Na Gurian Adolf
Nkasi
kuu wa Mkoa wa Rukwa Zelote Stephen amewaonya wale wote wanaoendelea na suala la kuwatetea wanafunzi wanaopata mimba mkoani humo kuwa warudishwe shule na kusema kuwa suala hilo halipp kwani ni msimamo wa serikali ya awamu ya tano.
Ameyasema hayo alipofanya ziara kujionea maandalizi ya mapokezi ya wanafunzi wa kidato cha tano katika shule mbili za Wilaya ya Nkasi kwa muhula wa mwaka 2017/2018, ambapo kwa Mkoa wa Rukwa wanafunzi 1,155 wamepangiwa kujiunga na shule 13 zinazochukua wanafunzi wa kidato cha Tano. 
Mkuu huyo wa Mkoa alisema kuwa kwa Mkoa wa Rukwa pekee kuna kesi 165 za wanafunzi kupata mimba tangu Januari hadi Juni mwaka huu na kesi zao zinaendelea kushughulikiwa ili kuwapata watuhumiwa na kuwachukulia hatua.
“Katika Mkoa wangu huu adui yangu namba moja ni yule ambae anampa mtoto wa kike mimba na yeyote anayetetea masuala yanayozunguka mimba, tusije tukaruhusu watu ambao wameshafanikiwa na watoto wao kielimu halafu wanakuwa kwenye majukwaa ya kuwaharibia watoto wa wazazi wengine, shule siyo Clinic wala siyo Maternity, wanafunzi hawaji shuleni kupata mimba ni kusoma tu,” alisema Zelote 
Sambamba na hilo aliwataka wazazi wote kukemea vitendo  vinavyolenga kukatisha ndoto za wanafunzi ambao wanaandaliwa kuijenga Tanzania ya viwanda, na kuongeza kuwa watoto ni wa watanzania si lazima awe wa kumzaa hivyo inampasa kila mzazi kuwa na uchungu pale anapoona mtoto wa mwenziwe amekatishwa ndoto zake kwa kupata ujauzito.
“Kwa wazazi na watu wazima hili lazima tulisimamie wote, mzazi, mtu mzima akimwona mtoto anafanya kitu kibaya achukue hatua, akemee na sio kupiga makofi na kutetea,” Alisema.
Katika kulisisitiza hilo Zelote aligawa nakala ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Namba 2 ya mwaka 2016 ambayo katika kifungu 60A (1 – 4) imebainisha adhabu kwa watu wanaowapa mimba au kuoa ama kuolewa na mwanafunzi, kwa kifungo cha miaka 30 jela.
Awali akisoma taarifa fupi ya hali ya mimba katika Shule zilizopo Wilaya ya Nkasi Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Nkasi Abel Adam Ntupwa alisema kuwa wananchi na wazazi wengi hawaifahamu sharia ya elimu inayotaka mwanafunzi akipata mimba taarifa na vielelezo vinapelekwa kwa afisa mtendaji kata au Kijiji na kesi kupelekwa polisi kisha mahakamani.
“Baadhi ya wazazi na watendaji wanakula njama ya kutaka kumaliza kesi kienyeji kwa wazazi wa pande mbili kupatana, hivyo uongozi wa wilaya utatoa elimu pana juu ya haki ya msichana kusoma mpaka kumaliza na kuwachukulia hatua wale wanaosaidia kuficha wahalifu wa mimba,” Alisema. 
Katika kuonesha umakini wa kulifuatilia suala hilo Afisa Elimu wa Mkoa wa Rukwa Robert Nestory alisisitiza kuwa upimwaji mimba kwa wanafunzi ufanywe mara kwa mara isiwe tu wakati shule zinapofunguliwa.
Alisema utaratibu wa kuwapima mimba wanafunzi wakati shule zinapofunguliwa tuuache, upimwaji huu uwe ni wa mara kwa mara, na maafisa elimu wanapokwenda kutembelea shule mbali mbali basi ni jukumu lao kuonana na wazazi ili wawape elimu ya sheria hii na sio tu kumuachia Mkuu wa Wilaya kazi hiyo.
Wakati akimkaribisha Mkuu wa Mkoa,Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Said Mtanda alibainisha mpango wa kuwatangaza kwenye redio watuhumiwa wote ili jamii isikie na kuondoa dhana ya kuwaficha katika maeneo yao wanayoishi.
“Orodha yao watuhumiwa wote tunayo na redio tunayo, Nkasi FM, tutawangaza kwa majina ili wafamu kwamba wanatafutwa ili kuwatia hofu hasa maeneo ya huku vijijini,” alisema Mtanda
Mwisho

No comments:

Post a Comment