Wednesday 12 July 2017

Ole wake atakae hujumu ushirika

Na  Gurian Adolf
Katavi
 Serikali  ya Mkoa wa Katavi  imeonya kuwa  kamwe haipo tayari kumfumbia macho mtu awaye yeyote yule atakae onyesha  nia ya kuhujumu  vyama vya  Ushirika  kwani  lengo la  mkoa huo ni kuendelea kusimamia  ushirika  imara  na  wenye  nguvu  ya kiuchumi  kwa kuwahudumia  wanachama  wake  kikamilifu.
Onyo  hilo  lilitolewa jana  na  Mkuu wa  Mkoa huo Meja  Jenerali  mstaafu  Raphael  Muhuga  wakati akitoa hotuba  yake  katika uzinduzi  wa jukwaa la Ushirika Mkoa wa  Katavi  iliyosomwa  kwa   niaba yake na  Katibu Tawala wa  Mkoa huo Kamishina wa  Polisi  Paulo   Chagonja  uliofanyika  katika  ukumbi wa Idara ya  Maji mjini  humo.
 Alisema  kuwa Serikali  Mkoani  Katavi   itaendelea kusimamia  ushirika  na kamwe  haitamfumbia  macho   mtu yeyote    atakae onyesha  nia  ya  kuhujumu   vyama  vya  Ushirika kwa namna  yoyote ile. 
 Lengo  la Mkoa  wa  Katavi  ni kuendelea  kuwa  kinara  kwa kuwa na  ushirika  imara   na  wenye   nguvu  kiuchumi  kwa kuwahudumia wanachama  wake  kikamilifu.
 Alisema  kumekuwa  na  malalamko  kwa  baadhi ya  vyama  vya ushirika  yanayosababishwa  na udhaifu  katika  uendeshwaji  wa  vyama  vya ushirika  na  udhaifu  huo  umetokana  na usimamizi   hafifu, kukosekana  kwa uaminifu  kwa  baadhi ya  viongozi  na  kukosekana  kwa uwazi  wa utoaji wa taarifa  kwa wakati.
Chagonja alitoa  rai  kwa  viongozi  wa  ushirika wa  mkoa huo kufanya  kazi  kwa bidii,waledi uaminifu  na uadilifu katika  utendaji  wa kazi  ili   mapungufu  hayo  yalioonekana   yasitokee  tena.
Mkuu  huyo wa  Mkoa   alisema  kuwa  kilimo  cha   Tumbaku   kimeanza   kuwa  na   changamoto   mbalimbali  ikiwa  ni  pamoja   na kupungua  kwa  soko   au    mahitaji  kutoka kwa   makampuni  ya ununuzi  na  chamgamoto ya utunzaji wa  mazingira  kwa kupanda miti   ambapo Serikali   imeelekeza  kuwa kila   mkulima   apande  miti 150  katika  shamba   lake   binafsi na kuitunza   miti ya  asili  aina ya NIGITRI 200.
Kwaupande wake naibu mrajisi wa vyama vya  ushirika  Tanzania   Charles  Malunde  alieleza kuwa   vyama  vya  ushirika   vinaweza  kufa au kuporomoka kabisa endapo  viongozi wanao ongoza ushirika huo  watakuwa ni wabovu.
Naibu  Mrajisi aliwaeleza wajumbe wa  mkutano huo wa jukwaa  la ushirika  kuwa  kila  mkoa   unachangamoto  za  ushirika  wapo  baadhi ya watu  wakiambiwa ushirika wanajua  umeisha kufa  na   wengine wanajua kuwa Sacos  sio ushirika.
Nae   Mrajisi  Msaidizi  wa    Vyama  vya  ushirika  wa   Mkoa wa   Katavi    Luhigiza    Sesemkwa   alisema kuwa  kumekuwa na  tabia  ya  baadhi ya viongozi  wa kisiasa kuingilia  shughuli  za  vyama  vya ushirika  na kufanya maamuzi  bila kuzingatia   sheria  na   taratibu  za ushirika.
 Alisema kuwa  mwamko   mdogo  kwa   wananchi  katika  kujiunga  na ushirika  ikizingatiwa   idadi ya  wakazi wa  Mkoa wa  Katavi  ni  671,194  ambapo   wanachama  wa ushirika  ndani ya  Mkoa   ni 16,000 tu ambao  ni sawa  na  asilimia 2.8 ya wananchi  wote wa    Mkoa  wa   Katavi  kwa  mujibu wa   sensa ya mwaka 2012.
Naye Mwenyekiti wa  chama  cha   Msingi cha  Nsimbo  Maganga    Kasea   alizilalamikia  Halmashauri kwa  kushindwa  kutengeneza  miundo mbinu ya   barabara kwenye   maeneo yanayozalisha  Zao la tumbaku  licha ya  kuwa wanapata   fedha   nyingi zitokanazo  na ushuru wa   Tumbaku    ambapo   asilimia   5  ya  thamani  ya  fedha za  mauzo ya tumbaku  huenda  kwenye  Halmashauri husika.
  Katika   uzinduzi wa   jukwaa la   ushirika   Mkoani    katavi    wajumbe wa   mkutano huo   walifanya uchaguzi mkuu na kumchagua   Moses   Kabeja  kuwa   Mwenyekiti  wa   jukwaa  la ushirika  la  mkoa wa  Katavi  baada ya kuwashinda  wagombea  watano wa  nafasi  hiyo na   Makamu   Mwenyekiti   alichaguliwa  Suzana   Kasera  aliyewashinda  wagombea   wanne wa  nafasi   hiyo.
Mwisho

No comments:

Post a Comment