Na Israel Mwaisaka
Nkasi
MAHAKAMA ya hakimu mkazi wa wilaya
ya Nkasi mkoani Rukwa imemuhukumu kifungo cha miaka miwili jela Augustino
William mkazi wa kijiji cha kirando baada ya kupatikana na kosa la kujiita meneja
wa shirika la kuzalisha umeme(TANESCO) wilaya ya Nkasi na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kutoka kwa wakazi wa kijiji cha
Kirando kinyume cha sheria.
Hukumu hiyo ilimetolewa na hakimu
mkazi wa wilaya ya Nkasi Lilian Lutehangwa baada ya
kusikiliza shauri hilo kwa ushahidi wa upande mmoja na kuridhishwa pasi na
shaka yoyote kuwa mtuhumiwa Augustino
William alitenda kosa kwa makusudi na
kutoa hukumu hiyo kwa kuzingatia kifungu cha adhabu cha 35 cha kanuni ya adhabu
na kumuhukumu kifungo cha miaka miwili
jela ili kutoa fundisho kwa wenye tabia
ya namna hiyo na kuwa kifungo kitaanza atakapopatikana kwani mtuhumiwa hakuwepo
mahakamani hapo kwa taarifa kuwa aliruka dhamana.
Afisa Usalama wa TANESCO mkoa wa
Rukwa, Wilbroad Ndunguru ameelezea
kuridhishwa kwake na hukumu hiyo kwani kumekuwa na wimbi kubwa la vishoka ambao
wamekuwa wakiwatapeli wananchi wengi hasa maeneo ya vijijini na kuwalipisha
pesa kinyume cha utaratibuwa TANESCO.
Ndunguru amesema katika mkoa wa
Rukwa shirika limekuwa likipokea malalamiko mengi kutoka kwa wateja wake ambapo
tayari wameshaanza kuwafikisha mahakamani wanaobainika kuwarubuni wananchi kuwa
wao ni wafanyakazi wa shirika hilo ili kuondoa kabisa vishoka katika mkoa wa
Rukwa.
Baadhi ya wananchi waliokuwepo
katika eneo la mahakama wameeleza kuridhishwa na hukumu hiyo wengine wakiomba adhabu
iongezwe kutokana na kitendo cha kuwatapeli wananchi wanaojitahidi kujikwamua
kutokana na lindi la umasikini lakini wachache wanapita katika maeneo yao na
kuwarubuni kuwa ni wafanyakazi wa TANESCO kwa ahadi ya kuwapatia huduma ya
umeme.
No comments:
Post a Comment