Thursday 13 April 2017

Wakristu wagombea eneo la mazishi

Gurian  Adolf
Nkasi
WAUMINI wa madhehebu ya Kikristu katika kijiji cha Nkana wilayani Nkasi mkoani Rukwa wameingia katika mgogoro mkubwa kutokana na kugombania eneo la kuzikia katika kijiji hicho.
Wakristu hao ambao ni wa makanisa ya Romani Katoliki, Moravian na Assembliss of God wamejikuta wakivutana vikali kutokana na kugombea eneo la makaburi ambalo kanisa Katoliki wamekuwa wakidai ni mali yao hivyo waumini wa makanisa mengine hawapaswi kuzikwa katika makaburi hayo pindi wanapo fariki dunia.
Akizungumza na Nipashe mwenyekiti wa kijiji hicho Norbeth Pahali alisema kuwa mvutano huo umekuwa ni wa muda mrefu sasa ambapo uongozi wa kijiji na kata umeshindwa kuutatua kutokana na pande hizo kutotaka suluhu.
Alisema kuwa February 20 aliitisha mkutano wa hadhara kijijini hapo kwa lengo la kujadili namna ya kutatua mgogoro huo lakini mkutano huo ulivurugika na kulazimika kuuahirisha kutokana na vuta nikuvute iliyojitokekza kwa viongozi wa madhehebu hayo katika kijiji hicho.
Pahali alisema kuwa viongozi wa kanisa Katoliki kijijini hapo wamekuwa wakidai kuwa hawataki madhehebu mengine wakawazike waumini wao katika makaburi hayo pindi wanapofariki kwakuwa makaburi hayo ni mali yao kwani kanisa hilo ndilo kongwe kijijini hapo na lilianzisha makaburi hayo, hivyo madhehebu mengine nao wakatafute makaburi yao.
Mwenyekiti huyo wa kijiji cha Nkana alisema kuwa yeye aliwashauri waumini wa madhehebu nyingine waende mahakamani kwani suala hilo walikwisha lifikisha ngazi ya kata lakini nayo imeshindwa kutatua mgogoro huo ambao usipopatiwa ufumbuzi huenda ukapelekea hata uvunjifu wa amani.
Hata hivyo Gazeti hili liliwasiliana na mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Nkasi Julius Kaondo alisema kuwa ofisi yake haijapokea suala hilo lakini aliahidi kulifuatilia na kulipatia ufumbuzi haraka iwezekanavyo.
Alisema kuwa yeye binafsi haoni sababu kwanini kuibuke mvutano huo wakati madhehebu hayo yote ni ya Kikristu ambayo yanatofautiana tu misingi ya ibada lakini imani yao ni moja hivyo ni lazima busara itumike ili kutatua mgogoro huo ambao unaweza kukua iwapo ukifumbiwa macho.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa kazi ya dini ni kusisitiza amani, itakuwa ni ajabu iwapo viongozi wa madhehebu hayo watashindwa kuafikiana na kusababisha uvunjifu wa amani kwani ni wajibu wao kuilinda amani na sikuwa chanzo cha mgawanyiko.
Mwisho

No comments:

Post a Comment