Dar es Salaam.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza ratiba ya Uchaguzi Mkuu kwamba Agosti 21, mwaka huu itakuwa ni siku ya uteuzi wa wagombea urais, ubunge na udiwani.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari juzi,
Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu, Damian Lubuva (pichani) alisema tume
hiyo imetoa ratiba hiyo kwa mamlaka iliyopewa na sheria. “Tume inapenda
kuviarifu vyama vya siasa na wananchi wote kuwa ratiba hii inatolewa kwa
mamlaka iliyopewa kwa mujibu wa vifungu vya 35 B(1), 3(a), 37(1) (a) na
46 (1) vya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi.
Lubuva alisema vyama vya siasa vitafanya kampeni za uchaguzi kwa siku 64 kuanzia Agosti 22 hadi Oktoba 24, mwaka huu.
Jaji Lubuva alisema siku ya kupiga kura itakuwa Oktoba 25 kama Katiba ya Jamhuri ya Muungano inavyosema.
Katiba inasema Uchaguzi Mkuu utafanyika Jumapili
ya mwisho wa mwezi Oktoba ya mwaka wa tano tangu ulipofanyika Uchaguzi
Mkuu wa mwisho.
Wakati tume ikitangaza ratiba, vyama vya siasa
vimeanza mchakato wa kupata viongozi wa ngazi mbalimbali huku CCM na
Chadema vikitangaza siku ya kupata wagombea urais kupitia vyama vyao.
Juzi, CCM iliweka ratiba ya kupata viongozi ndani ya chama hicho na
ikatangaza kuwa kuwa Julai 12, mwaka huu mgombea urais kupitia chama
hicho atajulikana.
Chadema pia kimeshatangaza ratiba ya uchaguzi
ndani ya chama hicho kuwa mgombea urais atajulikana Agosti 4, mwaka huu.
Mgombea huyo ataingia kwenye kinyang’anyiro cha kumtafuta mgombea wa
vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Chama cha Tanzania Labour (TLP), kimeshamteua,
Macmillan Lyimo kuwa mgombea wake wa urais katika Uchaguzi Mkuu
utakaofanyika Oktoba mwaka huu. Lyimo alipitishwa kuwania nafasi hiyo
katika Mkutano Mkuu wa Taifa wa chama hicho uliofanyika jijini Dar es
Salaam.
Kwa upande wa chama cha NCCR - Mageuzi, fomu za
kugombea nafasi mbalimbali za uongozi zimeanza kutolewa na Mkuu wa Idara
ya Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Dk George Kahangwa amechukua fomu
za kugombea urais.
No comments:
Post a Comment