Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari, nyumbani kwake, Dodoma jana.
Dodoma.
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa hana mpango wa kuhama Chama Cha Mapinduzi (CCM) na iwapo kuna mtu anamchukia ndani ya chama hicho, ni vyema akahama kwa sababu yeye hana mpango huo.
Lowassa alitoa kauli hiyo alipozungumza na
wahariri wa vyombo vya habari nyumbani kwake mjini Dodoma jana ambako
alieleza mambo mbalimbali kuhusu afya yake, suala la Richmond, elimu,
ajira, utajiri wake na hali ya kisiasa kwa ujumla.
Hata hivyo, Mbunge huyo wa Monduli hakutaka kujibu
maswali mengi kwa madai kuwa atazungumza Jumamosi mjini Arusha
atakapotangaza nia yake ya kugombea urais.
Kuhama CCM
Alipoulizwa iwapo yupo tayari kuhama CCM na kwenda
upinzani asipopitishwa na chama hicho kuwania urais alisema: “Sina
mpango wa kuhama chama changu, sina plan B, mimi ni plan A tu, tangu
nimemaliza Chuo Kikuu mwaka 1977 nimekuwa mwana-CCM, sijafanya kazi nje
ya CCM ukiondoa miaka ambayo nilikuwa vitani Uganda na nilipohamishiwa
Kituo cha Mikutano cha Arusha (AICC). Maisha yangu yote yapo CCM.
“Kama kuna mtu ambaye hanitaki ndani ya CCM, yeye ndiye ahame, siyo mimi,” alisema.
Kimya miaka saba
Lowassa aliyejiuzulu uwaziri mkuu mwaka 2008
kutokana na kashfa ya mtambo wa kufua umeme wa Richmond, alisema kimya
chake baada ya tukio hilo kilitokana na siasa nyingi za uhasama na
kutishiana.
“Kwa miaka saba, niliona ni hekima kunyamaza,
askofu mmoja alinifundisha kuwa ukimya ni hekima kutoka kwa Mungu.
Nilichagua kuwa kimya. Nilinyamaza kwa sababu ilikuwa salama kunyamaza,
ningezungumza ningeweza kutibua mambo kwenye nchi na kusababisha mambo
ambayo hayapo.
“Nilinyamaza ili kuipa muda Serikali ifanye kazi
yake.... sikupenda kuzungumza kwa sababu ya siasa nyingi za uhasama na
kutishiana kwingi, kuna kusingiziana kwingi, kufitiniana kwingi. Kukaa
kimya ni jambo gumu sana kwa mwanasiasa, lakini nashukuru Mungu niliweza
hilo,” alisema Lowassa ambaye Jumamosi atatangaza nia ya kuwania urais
mjini Arusha.
Wagombea wapime afya
Wagombea wapime afya
Alipoulizwa kuhusu madai kuwa afya yake inaterereka, alisema anaamini yupo fiti na akashauri wagombea urais wote wakapimwe.
“Hata nikikimbia kilomita 100 watasema mimi
mgonjwa. Hivi karibuni nilitembea kilomita tano na albino jijini Dar es
Salaam, kuna watu wakasema nimechoka sana, nimepata ‘stroke’ na
nimekimbizwa Ujerumani kutibiwa, huo ni upuuzi mtupu. Kuna chuki
imeingia katika siasa zetu na kutakiana mabaya. Afya ni neema kutoka kwa
Mungu tu. Napenda kuwahakikishia kuwa nipo fiti na nipo fiti na kwa
lolote. Nadhani ni wakati sasa kwa chama chetu waweke utaratibu
wanaogombea nafasi hii ambayo nitaitangaza Jumamosi, tukapime wote afya
na mimi nitakuwa wa kwanza kujitokeza kwenda kupima.
No comments:
Post a Comment