.Muswada huo ulioandaliwa na Serikali na ulitakiwa kuwasilishwa katika kikao kilichopita kwa hati ya dharura jambo ambalo halikuwezekana baada ya kupingwa na wadau na baadhi ya wabunge.
Dar es Salaam.
Chama cha Wamiliki wa vyombo vya Habari Tanzania (Moat) kimeunda timu maalumu itakayokwenda bungeni Dodoma kuwashawishi wabunge wasiupitishe muswada wa sheria wa vyombo vya habari baada ya kubaini umejaa kasoro.
Muswada huo ulioandaliwa na Serikali na ulitakiwa
kuwasilishwa katika kikao kilichopita kwa hati ya dharura jambo ambalo
halikuwezekana baada ya kupingwa na wadau na baadhi ya wabunge.
Hata hivyo, muswada huo uliorejeshwa kwa wadau
kujadiliwa, unatarajiwa kupelekwa kwa mara nyingine katika kikao cha
Bajeti kinachoendelea ingawa si kawaida kwa Bunge la Bajeti kujadili
miswada ya sheria.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam
jana, Mwenyekiti wa Moat, Reginald Mengi (pichani) alisema baada ya
kuusoma, wamegundua kuwa kuna kasoro nyingi na miongoni mwake ni adhabu
kwa waandishi wa habari ambazo zitawafanya wawe waoga katika kufanya
kazi yao.
Alisema wadau wa habari na wataalamu wa sekta hiyo
wataendelea kuwaelewesha wabunge juu ya masuala mbalimbali yaliyomo
katika muswada huo ili hata wanapoupitia wawe na uelewa wa kutosha wa
kitu wanachotaka kukipitisha kuwa sheria rasmi.
Alisema licha ya kasoro hizo, pia kuna hila za
kuupitisha kwa haraka kusudi wasitoe mawazo yao juu ya vipengele kadhaa
ambavyo vinafinya uhuru wa vyombo vya habari na hata uhuru wa wananchi
kupata habari.
“Wanasiasa hawa walitumia sana vyombo vyetu vya
habari wakati wakitafuta kura na sasa wameshapata uongozi wanatuona
hatufai badala yake wanataka kutukandamiza kwa kutuwekea sheria nzito,”
alisema Mengi.
“Huu muswada ukipita, utakuwa ni sheria mbovu
ambayo haina manufaa kwa nchi yetu, pia Watanzania watakosa habari za
uhakika kwani ikiwa kila ufikapo muda wa taarifa ya habari saa 2.00
usiku wote wanalazimika kutazama Televisheni ya Taifa, sasa hii ndiyo
nini?” alihoji.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communications
Ltd, Francis Nanai alisema ni vyema magazeti yakatumia nafasi iliyopo
kuandika makala maalumu kila siku kuhusu muswada huo ili wananchi wajue
matatizo yake.
Alisema pia wamiliki na waandishi wote wa habari
kwa pamoja wajiunge na wanaharakati wanaotaka kwenda mahakamani kuupinga
muswada huo ambao ni aibu kwa Taifa.
“Ni vyema muswada ukafanyiwa kazi baada ya uchaguzi wa Oktoba na rais ajaye ndiye auhalalishe kwa kutia saini,” alisema.
Mkurugenzi wa Sahara Media Group, Samwel Nyala
alisema suala la kulazimishwa kupeleka taarifa zao kwenye runinga ya
Taifa, kila saa mbili usiku ni kuwanyima wadau wa habari haki ya
upatikanaji wa habari.
No comments:
Post a Comment