Kwa ufupi
- Makongoro Nyerere asema sasa anajisikia kuomba nafasi ya urais
- Maprofesa Mwandosya, Muhongo kutangaza nia wiki ijayo
- Wafuata nyayo za Lowassa, Membe, Mwigulu, Makamba na Kigwangalla
Ni dhahiri sasa kuwa hatua ya vikao vya juu vya CCM kuwafungulia makada wake waliokuwa wamefungiwa kwa kuanza kampeni mapema na kutangaza tarehe za kuanza kuchukua fomu, vimechochea harakati za kusaka urais na kuongeza urefu wa foleni ya wanaotaka kuelekea Ikulu kumrithi Rais Jakaya Kikwete.
Hayo yamejitokeza ndani ya siku nne baada ya
uamuzi huo wa CCM kutangazwa mjini Dodoma na kuwafanya makada wake,
kuanza kujitokeza hadharani wakiweka bayana tarehe za kutangaza nia
hiyo.
WanaCCM waliojitokeza ni mtoto wa Baba wa Taifa,
Mwalimu Julius Nyerere, Makongoro Nyerere, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
(Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya na Mbunge wa Kuteuliwa, Profesa
Sospeter Muhongo ambao kwa nyakati tofauti wamethibitisha kuwa
wanatangaza nia hiyo wiki ijayo.
Wakati Makongoro akisema sasa anajisikia kuomba
kazi ya urais na anatarajia kutangaza nia hiyo kabla ya Juni 3, Profesa
Muhongo ameahidi kufanya hivyo kati ya Mei 31 na Juni 3, huku Profesa
Mwandosya akisema ataweka wazi kila kitu Jumatatu ijayo. Tarehe ya
kuanza kuchukua fomu kwa chama hicho ni Juni 3 na kurejesha ni Julai 2.
Kuingia ulingoni kwa mada hao ambao kwa muda mrefu
hawakuwa tayari kuzungumzia suala hilo, kunaongeza orodha ya makada
waliokwishajipanga kwenye foleni hiyo akiwamo Waziri Mkuu wa zamani,
Edward Lowassa anayetarajia kutangaza kile anachoita ‘safari ya
matumaini’ Jumamosi mjini Arusha, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa, Bernard Membe aliyetangaza nia hiyo juzi, akifafanua kuwa
atafanya hivyo hivi karibuni huko Mtama, Lindi alikozaliwa.
Pia wamo, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika,
Stephen Wasira aliyekwishaeleza nia hiyo, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu
Nchemba aliyejiuzulu unaibu Katibu Mkuu wa CCM Jumapili ili aweze
kuwania urais bila mgongano wa masilahi katika vikao vya chama hicho,
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, Mbunge wa Nzega, Dk
Hamis Kigwangalla, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia,
January Makamba na Balozi wa Kudumu wa Umoja wa Afrika (AU) katika
Umoja wa Mataifa (UN), Amina Salum Ali.
Katika mlolongo huo wapo makada waliokuwa
wanatajwa muda mrefu ambao wanasubiriwa kuweka bayana ni hiyo ambao ni
Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye na Mbunge wa Sengerema, William
Ngeleja.
Kauli ya Makongoro
Akiwa mjini Mbeya juzi, mbunge huyo wa Afrika
Mashariki alisema: “Najisikia kuomba kazi ya kuwaongoza Watanzania
katika ngazi ya juu ya uongozi, kwani uwezo ninao, afya na muda wa
kufanya hivyo vinaniruhusu.”
Makongoro alisema hayo wakati akitoa shukrani kwa
viongozi wa dini baada ya kumkabidhi Tuzo ya Kumbukumbu ya Mwalimu
Nyerere kwa niaba ya familia, ikiwa ni ishara ya kuenzi na kukumbuka
kazi alizofanya Baba wa Taifa enzi za uhai wake.
Awali, viongozi wa dini na machifu walioshiriki
hafla hiyo, walimtaka Makongoro ‘kuvunja tetesi’ zinazosambazwa kupitia
vyombo vya habari juu yake kuhusu kuwania urais na kumtaka atamke wazi
juzi hilo kwa kuwa wako tayari kumsaidia katika harakati zake.
Kiongozi wa machifu wa Busokelo, Prince Mwaihojo
alisema wananchi wa Mbeya wana imani kubwa na familia ya Mwalimu Nyerere
kwa kuwa mwasisi huyo wa Taifa alikuwa akitangaza mambo mazito akiwa
mkoani hapo.
No comments:
Post a Comment