Tuesday, 5 December 2017

Serikali yaagiza kumaliza tatizo la madarasa nchini

Na Israel Mwaisaka
Nkasi
SERIKALI imewaagiza wakuu wa wilaya zote nchini  kuhakikisha wanamaliza tatizo la uhaba wa vyumba vya madarasa ili wanafunzi wanaofaulu sambamba na kuanza masomo wasikose nafasi kutokana na uhaba wa madarasa. 
Naibu waziri wa Tamisemi Josephat Kandege alitoa agizo hilo jana alipokuwa akizungumza na watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Nkasi ambapo pia aliupongeza uongozi wa wilaya hiyo kwa kufanikiwa kujenga vyumba vipya 580 vya madarasa kwa kuwashirikisha Wananchi.
Alisema hivi sasa kuna wanafunzi waliomaliza darasa la saba na wanatakiwa kujiunga na masomo ya sekondari mapema mwakani lakini kuna changamoto kubwa ya nafasi hasa kwa kukosekana kwa vyumba vya kutosha vya madarasa na kuwa ni lazima kila wilaya ihakikishe inafanya liwezekanalo kuhakikisha Wanafunzi wote waliofaulu kwenda sekondari wanaendelea na masomo.
Naibu waziri alisema kuwa katika taarifa ya wilaya ya Nkasi iliyotolewa na mkuu wa wilaya hiyo Said Mtanda inaonesha kuwa waliweka mikakati kwa kila kijiji kuhakikisha wanajenga vyumba vitatu vya madarasa katika mwaka huu na ni mpango ambao ni endelevu kwa kila mwaka na kuwa kwa kufanya hivyo wilaya imejikuta ikipunguza kwa kiasi kikubwa tatizo hilo la uhaba wa nafasi za kusomea  wanafunzi waliofaulu.
Alisema wilaya nyingi nchini kilio  chao kikubwa ni uhaba wa  madarasa na kuwa sasa Wakuu wa wilaya wote waende wilayani Nkasi  kujifunza namna wao walivyofanikiwa katika eneo hilo.
Sambamba na hilo Kandege ameitaka halmashauri ya Nkasi kuhakikisha  inaondoa changamoto zinazowakabili watumishi hasa za kupanda vyeo kwa wakati ikiwa ni pamoja na stahiki zao ili kuweza kuwapa mori katika kufanya kazi na kuleta tija.
Awali mkuu wa wilaya  ya Nkasi, Mtanda alimweleza Waziri huyo namna wanavyokabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo ya vyumba vya madarasa na kumuhakikishia kuwa hakuna mwanafunzi  atashiyendwa kuendelea na masomo kwa sababu ya uhaba wa madarasa na Kuongeza kuwa  wameanza mkakati  ifikapo januari mwakani tatizo hilo liwe limetafutiwa ufumbuzi.
Naibu Waziri pia ameweza kutembelea ujenzi wa majengo mapya ya  kituo cha afya cha Nkomolo katika suala zima la kuimarisha huduma za afya,ikiwa ni pamoja na kutembelea Mwalo wa kuuzia samaki wa Kirando uliojengwa na serikali.
Mwisho        

No comments:

Post a Comment