Saturday, 2 December 2017

Rc aiagiza idara ya elimu

Na Gurian Adolf
Nkasi 
MKUU wa mkoa Rukwa Joakhimu Wangambo ameiagiza idara ya elimu wilayani Nkasi kuhakikisha kuwa wanafunzi wote waliofaulu darasa la saba wanapata nafasi ya kuingia kidato cha kwanza mwakani.
Agizo hilo alilitoa jana kwenye kikao cha halmashauri kuu ya CCM wilaya kilichokuwa kikipokea taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ambapo alimuagiza mkuu wa wilaya ya Nkasi Said Mtanda kuhakikisha kuwa wale wote waliofaulu mwezi januari wanaanza masomo ya sekondari.
Alisema wilaya hiyo imefikisha ufaulu wa asilimia 74 na kushika nafasi ya pili kimkoa pamoja na uhaba wa vyumba vya madarasa ukilinganisha na idadi kubwa ya wanafunzi waliofaulu na kuiagiza serikali wilayani humo kuhakikisha kuwa hakuna mwanafunzi anayekosa nafasi ya kuingia kidato cha kwanza kwa kutokana na uhaba wa madarasa.
Alisema kama ufaulu huo umeleta shida ya madarasa endapo utafikia asilimia 100 hali itakua zaidi ya hapo na kuiagiza wilaya hiyo  jukumu la kuhakikisha wanafanya mbinu zozote  kuhakikisha wanafunzi wote wanajiunga na masomo ya sekondari na si vinginevyo.
“”Nilipata taarifa kuwa licha ya ufaulu huu lakini baadhi ya Watoto hawatapata nafasi ya kuendelea na masomo ya sekondari kutokana na ufinyu wa nafasi kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa sasa nasema sitaki kusikia kuwa kuna mtoto kakosa nafasi nataka viongozi wa wilaya mjiongeze””alisema
Sambamba na hilo alitaka kuwepo na mpango mkakati kwa kata 10 zilizopo mwambao mwa ziwa Tanganyika ambako kuna changamoto kubwa ya kuwepo kwa wahamiaji haramu wengi ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria na kuwataka kuingia nchini kwa kufuata sheria.
Aidha aliwataka Wananchi wa maeneo hayo ya mwambao  waelimishwe ili wajue ubaya wa kuwapahifadhi wahamiaji haramu na watambue kuwa kufanya hivyo wanafanya makosa kisheria.
Kwaupande wake mkuu wa wilaya hiyo Mtanda aliwasilisha taarifa ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi amabo wajumbe wa kikao hicho waliikubali taarifa hiyo kwa asilimia 100 na kutaka baadhi ya miradi inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali kuongeza juhudi ili iweze kukamilika  ili jamii iweze kunufaika na huduma za miradi hiyo.
Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa wao wamelisimamia kwa ukaribu suala zima la utendaji wa watumishi  ili uweze kuleta tija,na pale wanapobaini kuwa kuna kiongozi yeyote anapwaya katika eneo lake wanachofanya ni kumvua madaraka yake palepale alipo na si kumuhamisha kumpeleka mahali pengine na kuwa hilo limewezesha utendaji  kuimarika mahali pa kazi.
Naye mwenyekiti wa CCM wilaya ya Nkasi Privatus Yoramu aliwataka Watendaji wa chama wa ngazi zote kutoa ushirikiano kwa viongozi wa serikali hasa mkuu wa wilaya na mkurugenzi wakati wa kutekeleza majukumu yao ili waweze kuunganisha nguvu kwa pamoja katika kuleta ufanisi katika kuwahudumia wananchi.
Alisema uongozi wa serikali ya wilaya kutokana na unavyofanya kazi ipo haja ya kupewa ushirikiano wa kutosha ili wasipate vikwazo katika utendaji wao.
Mwisho

No comments:

Post a Comment