Na Gurian Adolf
Sumbawanga
WATOTO wa kike mkoani Rukwa wamepewa mafunzo maalumu ya namna ya kuzitambua changamoto mbalimbali zinazowakwamisha kuzitumia fursa zilizopo katika kutekeleza matarajio yao ili waweze kujitegemea.
Akizungumza katika uzinduzi wa mradi uitwao U-report unaotekelezwa na Tanzania Girl Guides Association mkufunzi wa mradi huo Emiliana Stanslaus alisema wahitimu wapatao 20 katika kila halmashauri wamewezeshwa namna ya kuwasaidia wasichana wenzao katika kukabiliana na vitendo vya ukatili dhidi yao.
Alisema wasichana hao walipata mafunzo ya siku mbili ambapo watawasaidia wanafunzi wenzao wa kike katika shule za msingi na sekondari na wasichana waliopo vijijini katika kukabiliana na changamoto mbalimbali katika maisha yao ikiwa ni pamoja na kubakwa na pia kupata mimba za utotoni.
Emiliana alisema mradi huo utatekelezwa katika halmashauri za Sumbawanga vijijini, Kalambo Nkasi na Sumbawanga Manispaa kwa njia ya kutuma ujumbe wa maandishi ya simu kwenda namba maalumu ya 15070 kwa mitandao yote na kuwawezesha walengwa kutoa taarifa kwenye vyombo na mamlaka zinazohusika dhidi ya vitendo vya ukatili walivyofanyiwa wasichana hao.
Alisema Tanzania Girl Guides Association kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa linalo shughurika na watoto ulimwenguni UNICEF- itatoa mafunzo kwa wasichana zaidi ya 15 elfu watakaosaidia kuwaelimisha wenzao katika mikoa ya hapa nchini namna ya kukabiliana na vitendo vya ukatili.
Naye Honorotha Wamai ambaye ni mkufunzi wa Girl Guides mkoa wa Rukwa alisema wasichana hao waliohitimu watakiwa kutoa mafunzo yanayohusu mradi huo katika halmasahuri zao za wilaya kwa kushirikiana na idara za elimu na maendeleo ya jamiii.
Awali akizindua mradi huo kwa niaba ya katibu tawala mkoa wa Rukwa mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga John Msemakweli alisema serikali imetunga sheria zinazowalinda wasichana dhidi ya vitendo vya ukatili.
Alisema katika utekelezaji wa sheria hizo serikali mkoani Rukwa itawafikisha mahakamani wazazi ambao watoto wao wanapata ujauzito pindi itakapo bainika kuwa wameshiriki kuficha ukweli au vielelezo vitakavyosaidia kuwatia hatiani watuhumiwa wa kuwapa mimba mwanafunzi.
Mwisho
No comments:
Post a Comment