Wednesday 1 November 2017

Washauriwa kutunza mazingira ili kuliokoa ziwa Rukwa


Na Gurian Adolf
Sumbawanga
WAKAZI wanaoishi kwenye bonde la ziwa Rukwa wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa wameshauriwa Kuongeza kasi katika huifadhi wa mazingira ili kuliokoa ziwa hilo lanalozidi kukabiliwa na hatari ya kukauka. 

Ushauri huo umetolewa jana na afisa ufuatiliaji na tathmini wa tasisi ya Kaengesa Environment Conservation Society(KAESO) Grace Shio wakati wa semina ya siku moja ya kuzijingea uwezo asasi za kiraia katika mikoa ya Rukwa na Katavi  ili ziweze kukabiliana na uharibifu wa mazingira katika mikoa hiyo. 

Alisema kuwa wakazi waishio katika bonde la ziwa Rukwa wanajukumu kubwa la kuhakikisha wanatunza mazingira ikiwa ni pamoja na kuacha tabia ya kukata miti hovyo,kupunguza mifugo na kulima mpaka kando ya ziwa hilo kwani vitu hivyo vimechangia kupungua kwa kina cha ziwa hilo sambamba na kupungua kwa ujazo wa maji. 

Shio alisema kuwa iwapo mambo hayo yataachwa bila kushughulikiwa  katika kipindi cha miaka 30 ijayo ziwa hilo litakauka na kupotea kabisa kwenye uso wa dunia kwani hali inazidi kuwa mbaya siku hadi siku. 

Alitoa wito kwa asasi mbalimbali zinazo jishughulisha na uhifadhi wa mazingira hapa nchini kulivalia njuga suala la mazingira katika  bonde la ziwa Rukwa kwani ni muhimu kwa shughuli za uvuvi,utaali na uwindaji kwakua linapakana na hifadhi taifa ya wayamapori ya Katavi na pia ni miongoni mwa maziwa machache yenye mamba wengi duniani. 

Kwaupande wake mmoja wa wajumbe wa warsha hiyo Mussa Mwangoka akichangia mada alisema kuwa changamoto kubwa iliyopo ni ukosefu wa  elimu sahihi ya uhifadhi wa mazingira  kwa wakazi waishio mwambao wa bonde la ziwa hilo.

Alisema iwapo  jamii ya wafugaji waliopo katika bonde hilo wataelimishwa namna ya kufuga kufuatana na eneo la malisho pamoja na wakulima kupewa elimu ya kuacha kulima mpaka karibu na ziwa hilo sambamba na elimu ya kulima katika miinuko kwani kunachangia udongo kusombwa na maji nyakati za masika na kuporomokea ziwani hivyo kufanya kina cha ziwa kuzidi kuwa kifupi,huenda ziwa hilo likasalimika. 

Hata hivyo wajumbe wa Warsha hiyo waliazimia kwa pamoja Kuongeza elimu kwa wakazi waishio katika bonde hilo kwani faida za ziwa hilo ni kubwa kwa mustakabali wa kizazi cha sasa na kijacho kwakua fursa ni nyingi na zinahitajika katika ziwa hilo. 

Mwisho

No comments:

Post a Comment