Wednesday 4 October 2017

Fuso laua 15

Na Israel Mwaisaka
Nkasi
WATU 15 wamefariki dunia na wengine 6 kujeruhiwa baada ya gari waliokuwa wakisafiria kuacha njia na kugonga mwamba na kisha kupinduka.
Ajali hiyo ilitokea juzi katika tarafaya Wampembe wilayani Nkasi wakati gari aina ya Fuso lililokuwa likitokea katika kijiji cha Wampembe kuelekea mjini Sumbawanga
 Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mkuu wa wilaya Nkasi Said Mtanda alisema kuwa ajali hiyo ilitokea  majira ya saa 9 alasiri katika eneo la mbuga nyeupe baada ya gari hilo kugonga Mwamba na kupinduka.
Alisema kuwa baada ya gari hilo kupinduka watu 12 walikufa papo hapo na wengine watatu walifariki baada ya kufikishwa katika hospitali ya mkoa Rukwa ya Sumbawanga wakiwa wanaendelea kupewa matibabu.
Mwenyekiti huyo wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya hiyo alisema kuwa dereva wa gari hilo alikuwa  ni mgeni alikuwa hajawahi kupita katika barabara hiyo na baada ya kufika katika eneo hilo ambalo huwa lina kona kali alishindwa  kumudu  gari na kwenda kugonga mwamba na hatimaye gari kupinduka kisha dereva kukimbia kutorokea kusikojulikana.
Alisema kuwa baada ya tukio hilo waliwakimbiza majeruhi katika hospitali ya mkoa huku maiti zote zikiifadhiwa katika kituo cha afya cha Mvimwa kwa ajili ya utambuzi wa ndugu zao.
Alisema kuwa Jana asubuhi wameketi kikao cha kamati ya ulinzi na usalama na kuteua gari moja la jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ambalo litatumika kusafiriisha maiti zote zitakazotambuliwa na ndugu zao hadi katika maeneo yao kwa ajiri ya mazishi.
Aidha amewataka Wananchi kujitokeza katika kituo cha afya cha Mvimwa kwenda kuzitambua maiti ili na kuwa gharama zote za usafirishaji wa maiti hizo hdi makwao zitabebwa na serikali.
Pia alimpongeza  mkuu wa mkoa Rukwa Kamishina mstaafu wa jeshi la Polisi Zelote Sitivini kwa  kufika mapema sana katika eneo la tukio na kushirikiana na serikali ya wilaya katika kushughulikia ajali hiyo ambayo ni kubwa kutokea wilayani Nkasi.
Hata hivyo kamanda wa polisi mkoani humo George Kyando alitoa wito kwa madereva kuwa makini wawapo barabarani ili kuepuka ajali zinazokatisha maisha ya wananchi. 
mwisho

No comments:

Post a Comment