Tuesday, 15 August 2017

billion 12.5 kusambaza umeme

Na Israel Mwaisaka
Nkasi
NAIBU Waziri wa Nishati na Madini  Dk,Medard Kalemani amemtaka mkandarasi wa kusambaza umeme vijijini REA kupitia kamouni ya Nakuroi Investment Company kuhakikisha kuwa wanaikamilisha kazi hiyo katika kipindi cha miaka miwili walichopewa na si vinginevyo ili wananchi waweze kuipata nishati umeme kwa wakati.
Agizo hilo alilitoa jana alipokuwa akizindua awamu ya tatu ya usambazaji umeme vijijini kupitia REA mkoani Rukwa katika kijiji cha Kabwe kata ya Kabwe wilayani Nkasi ambapo alisema kuwa serikali imewekeana mikataba na mkandarasi huyo wa miaka miwili kukamilisha kazi hiyo kinyume cha hapo watachukua hatua stahiki kwa maana watakua wameuvunja mkataba.
Alisema kuwa katika mpango wa sasa umeme unatarajia kwenda katika vijiji 111 na  zimetengwa shilingi Bilioni 12.5 na haoni sababu ya mkandarasi kushindwa kumaliza kazi hiyo katika kipindi hicho cha miaka miwili kama mkataba unavyoeleza.
Dk Kalemani alisema kuwa taasisi zote za serikali zilizopo katika vijiji zitapelekewa umeme huo ikiwa ni pamoja na mitambo yote ya maji itapelekewa umeme huo na kuwa watu wote wataunganishiwa umeme kwa shilingi 27,000 na si vinginevyo.
Awali mkurugenzi wa REA Mhandisi Gisima Nyamhanga aliwataka Wananchi kuepuka vishoka pale wanapotaka kuingiziwa umeme katika nyumba zao bali wafike kwenye ofisi za REA au katika ofisi za TANESCO ili kuweza kukabiliana na matapeli,lengo ni kutaka kuona wananchi wanapata umeme bila shida ili uweze kuchangia katika shughuli zao za kimaendeleo.
Mkurugenzi mtendaji wa TANESCO  Dk Tito Mwinuka kwa upande wake  aliwataka wakazi wa wilaya ya Nkasi na mkoa wa Rukwa kwa ujumla hususani waishio vijijini kujiandaa kuwa wateja wa TANESCO kwa kuhakikisha kuwa wanailinda vyema miundo mbinu ya umeme ili iweze kuwasaidia kama lilivyo lengo la serikali.
Alisema wao kama TANESCO watafurahi zaidi pale watakapoona umeme huo unabadilisha maisha yao kwa kuutumia katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na hasa Katika kuwekeza viwanda.
Wabunge wote wa majimbo ya Nkasi kusini na Kasikazini Desderius Mipata na Ally Kessy waliishukuru serikali kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuhakikisha umeme unafika hadi vijijini na kuwa uzinduzi wa awamu ya tatu ya REA unaleta matumaini na kuitaka jamii kuanza kujenga nyumba bora zitakazoendana na maendeleo ya umeme.
Mkuu wa wilaya Nkasi Said Mtanda aliwataka Wananchi wa wilaya Nkasi kuachana na tabia ya kuchoma moto misitu inayopelekea nguzo za umeme kuungua na kuharibu miundo mbinu ya umeme na kuwa sasa ataitisha kura ya siri ili kuwatambua watu wanaofanya vitendo hivyo vya kuchoma moto misitu ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
Alisema kila mmoja awe ni mlinzi wa mwenzake kwa kutoa taarifa pale wanapoona kuwa kuna watu ambao ni waharibifu wa miundo mbinu ya umeme ili wasiweze kuikosa huduma hiyo muhimu kwa maendeleo yao.
Wakazi wa kata ya Kabwe walionyesha furaha kubwa ya uzinduzi wa REA awamu ya tatu na kuwa sasa wana uhakika mkubwa kuwa umeme utafika kwao na kuwa wengi wao katika eneo hilo ni wavuvi ,hivyo watautumia umeme huo katika kusindika samaki na kuweza kuzipeleka kwenye masoko makubwa ili kuuza kwa bei kubwa na ile hofu ya samaki kuharibika itaondoka miongoni mwao.
mwisho

No comments:

Post a Comment