Tuesday 18 July 2017

Zaidi ya Bilioni 1.1 yaikarabati Kantalamba Sekondari

Na Gurian Adolf
Sumbawanga
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Zelote Stephen amewataka wale wote wanaohusika na usimamizi wa fedha za ukarabati wa moja ya shule Kongwe nchini, kuhakikisha kuwa fedha hizo zinatumika kama zilivyokusudiwa.
Aliyasema hayo baada ya kuzungukia maeneo ya shule hiyo yanayoendelea kukarabatiwa wakati alipofanya ziara ya kushtukiza ili kujionea hatua waliyofikia katika ujenzi na kutathmini kama thamani ya pesa inakwenda sambamba na ujenzi unaoendelea katika shule hiyo.
Shule ya Sekondari ya Kantalamba ni miongoni mwa shule kongwe 20 nchini ambazo serikali kupitia Wizara ya Elimu imeweka mpango wa kukarabati shule hizo kwa lengo la kutunza hadhi na kuziboresha zaidi. Ambapo shule hiyo imepata mgawo wa shilingi 1,123,353,700/=
“Tafadhalini sana Mwalimu Mkuu, Mkurugenzi, Afisa Elimu na sisi wote tuhakikishe kwamba shule hii imebadilika kwa kuwa hizi pesa si kidogo, bilioni sio hela kidogo, zisichezewe, zifanye kazi iliyokususdiwa na kazi yenyewe ioneshe sura ya bilioni, isijekutokea tukapata kazi nyingine ya kusema kwamba hizi pesa kazi iliyofanyika ni ya hovyo hovyo,” ...Alisisitiza.
Baada ya kuona juhudi zinazoendelea katika ukatabati huo  Zelote amesifu uongozi wa shule wa kuajiri mafundi vijana waliopo mtaani ili kuwa na matumizi mazuri ya fedha hizo tofauti na kuwatumia wakandarasi ambao wangesababisha fedha nyingine zipotee bila sababu, na kusisitiza kuwa vijana hao wasimamiwe kwa ukaribu na kupewa maelekezo ili wasilipue kazi inayoendelea. 
 Pamoja na hayo alilisisitiza uwazi kwenye matumizi ya fedha za umma, na kuwataka wakaguzi kuwa makini na kukagua kila hatua ya ujenzi na kuona kuwa kila senti inayotumika inaendana na thamani ya ujenzi inayoonekana
Aidha alizitaka Halmashauri zote Mkoani Rukwa kutenga bajeti kwa kupitia mapato yake ya  ndani ili kuboresha miundombinu ya shule jambo ambalo linaweza kubadilisha muonekano wa shule nyingi mkoani humo.
“Ningependa kuona shule hii inakuwa ya mfano kwakuwa ipo katika makao makuu ya mkoa na pia alishauri kujenga uzio na kuendeleza utunzaji wa mazingira kwa kuweka sharia kali kwa wanafunzi ili waendelee kutunza mazingira ya shule,”  aliongezea Zelote.
Awali akisoma taarifa fupi ya ukarabati wa shule kongwe Sekondari ya Kantalamba mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Martin Kasansa alitaja changamoto kadhaa zinazorudisha nyuma kasi ya ukarabati wa shule hiyo alisema ni uchakavu mkubwa wa bwalo uliosababisha kuanza upya ujenzi, upatikanaji wa baadhi ya vifaa mkoani Rukwa kuwa mgumu na kulazimika kuagiza kutoka mkoa wa Mbeya na kutopatikana kwa maji kumechelewesha ujenzi unaoendelea.  
“Kazi ya ukarabati ilianza rasmi mwezi June 2017 na inasimamiwa na muhandisi kutoka Chuo cha Sayansi na teknolojia Mbeya na inategemewa kumalika ndani ya miezi mitatu, lakini upatikanaji wa maji umekuwa ni tatizo katika eneo letu, ” Alisema
Ukarabati unaoendelea katika shule hiyo unahusisha mabweni 6, vyumba vya madarasa 14, ofisi za walimu, vyoo, mfumo wa maji safi na maji taka, mfumo wa umeme, jiko, bwalo, maabara pamoja na jengo la kilimo. Ambapo mapaka sasa Shilingi 648,051,540.90/= imeshatumika na kufikia asilimia Zaidi ya 58.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa Bernard Makali aliutaka uongozi wa shule kuangalia maeneo muhimu na kuweza kuyamalizia ili wanafunzi wasiachwe nyuma na muhula wa mwaka huu na kusisitiza kuwa upishi wa kutumia kuni si mzuri na kuahidi kushirikiana nao kutafuta namna ya kupikia kwa kutumia gesi jambo ambalo litatunza mazingira. 
Mwisho

No comments:

Post a Comment