Saturday 15 July 2017

Wafanyabiashara Sumbaeanga walilia milioni 14 zao

Na Gurian Adolf
Sumbawanga
Wafanyabiashara wa Soko la Mandela mjini Sumbawanga wameutaka uongozi wa Halmashauri ya Manispaa kueleza bayana hatma ya fedha zao kisia cha Sh milioni 14 walizochanga kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya soko hilo baada ya kuteketea kwa moto takribani miezi tisa iliyopita.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa vibanda vya soko hilo, Julius Bukuku alisema hayo jana wakati mkutano wa hadhara wa mbunge wa jimbo la Sumbawanga mjini, Aeshi Hilaly uliofanyika katika viwanja vya kata ya Malangali mjini hapa.
Alisema kwamba baada ya moto kuteketeza soko hilo na kusababisha hasara ya mamilioni ya fedha kwa wafanyabiashara hao, ndipo uongozi wa Manispaa hiyo ulipounda kamati ambayo ndani yake ilikuwa na watumishi wa halmashauri hiyo na baadhi ya wafanyabiashara lengo ikiwa ni kuchangisha fedha na kuboresha upya miundombinu ya soko hilo.
Bukuku alisema kamati hiyo ilifanikiwa kuwachangisha wafanyabishara hao fedha kiasi cha Sh milioni 14, ambapo wakati zoezi hilo likiendelea ofisi ya mkuu wa wilaya iliingilia kati na kusitisha uchangishaji huo.
Aliongeza kwamba baada ya kusitishwa kwa zoezi hilo, uongozi wa manispaa umekuwa kimya hakuna chochote kinachoendelea wala dalili za wafanyabiashara kurejeshewa fedha zao hazipo.
Alimuomba mbunge huyo kufuatilia ili kujua nini hatima ya fedha zao kwa kuwa ujenzi wa soko hilo umesitishwa na vitabu walivyokuwa vikitumika katika makusanyo hayo vipo mikononi mwa uongozi wa manispaa hiyo. 
Akijibu hoja hiyo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji  wa Manispaa ya Sumbawanga , George Lupilya  licha ya kukiri kufanyika kwa zoezi la ukusanyaji wa fedha hizo kwa wafanyabiashara lakini alidai kwamba mazungumzo yanaendelea kati ya uongozi wa halmashauri hiyo na chama cha Mapinduzi (CCM) ambao ni wamiliki wa eneo hilo.
Hata hivyo, Mbunge Hilaly alisema kwamba yeye afahamu kama kuna zoezi hilo linaendelea ila walichokubaliana katika vikao baada ya kuungua kwa soko hilo ni kutafuta fedha kutoka kwa wafadhili na wahisani mbalimbali ili wajenge soko la kisasa.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment