Tuesday 18 July 2017

Nkasi wajipanga kuongeza makusanyo ya ndani

Na Israel Mwaisaka
Nkasi
WATENDAJI wa halmashauri ya wilaya Nkasi mkoani Rukwa wametakiwa kuongeza jitihada kwenye makusanyo ya ndani ili kuweza kuyafikia malengo waliyojiwekea.
Wito huo umetolewa mwishoni mwa wiki na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya Nkasi Julius Mseleche Kaondo kwenye kikao maalumu cha kuweka mikakati namna ya kuongeza makusanyo ya ndani ambapo alidai kuwa bado kasi ya makusanyo hairidhishi na kinachotakiwa sasa ni kuongeza jitihada.
Katika kikao hicho kilichowajumuisha maafisa Watendaji kata na maafisa ugani pamoja na wakuu wote wa idara mbalimbali mkurugenzi aliwataka watendaji hao kuliona suala la makusanyo si la mchezo na kutaka kila mmoja kuongeza jitihada katika makusanyo ili kuiwezesha halmashauri kupata fedha za kuweza kuchangia shughuli za maendeleo ambazo zimeanzishwa na wananchi.
Alisema kuwa wilaya Nkasi ilikuwa inapigiwa mfano kwa wilaya zote mkoani Rukwa kwa makusanyo mazuri lakini sasa inaonekana kushuka na kumtaka kila mmoja sasa kuchukua hatua kwa kuongeza juhudi katika suala hilo la makusanyo.
Aliwasisitiza katika suala zima la uadilifu ambapo alidai kuwa serikali haitamuonea mtu huruma atakayekwenda kinyume na maadili na kuziiba fedha hizo na kuwa katika kipindi hiki  ukiiba fedha za serikali ni lazima utabainika na kuwa ni vizuri wakatanguliza uzalendo na uadilifu ili wasije wakakumbwa na mkono wa sheria
‘’uadilifu iwe ni kitu cha kwanza mnapokusanya mapato ya serikali na yeyote atakayethubutu kuiba fedha hizi mwisho wa siku atabainika na sisi tutachukua hatua stahiki papo hapo na kumfikisha mahakamani ili aweze kuadhibiwa’’alisema kaondo
Aliwataka watendaji hao kuwashirikisha Wananchi katika suala zima la ukusanyaji wa mapato na kuhakikisha kuwa kila Mwananchi anawajibika kwa kutoa taarifa pale wanapoona kuwa kuna mapato yanatoroshwa na wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu.
Mkaguzi wa ndani wa hesabu za serikali Freddy George kwa upande wake alidai kuwa suala la maadili ni la muhimu sana na kuwa wapo watendaji ambao sasa wameondolewa kazini sababu ya kutokuwa waadilifu kwenye fedha na kuwataka wao kuchukua hatua ili hayo yasije yakawakumba.
Afisa TEHAMA Francis Mkemwa alisema kuwa haoni sababu ya mapato ya halmashauri kushuka na kumtaka kila mmoja kujibidiisha na kuwa heshima ya wilaya itarudi kama zamani endapo kila mmoja atawajibika ipasavyo.
Naye afisa wa mamlaka ya mji mdogo wa Namanyere Vicent Magendera alidai kuwa  wilaya Nkasi ina kazi kubwa katika kuhakikisha kuwa wanasaidia nguvu za Wananchi zile walizozianzisha na kuwa ni fedha hizo hizo ndizo zitafanya kazi hiyo,hivyo ni jukumu la kila mmoja kuona kuwa kazi ya makusanyo ya halmashauri ni yake na kubwa ni la uadilifu.
Wilaya Nkasi kwa sasa ipo kwenye ujenzi wa vyumba vya madarasa ambapo kila shule inatakiwa kujenga vyumba vitatu vya madarasa na halmashauri jukumu lake ni kuhakikisha kuwa majengo hayo yanaezekwa kwa bati na mambo mengine
mwisho

No comments:

Post a Comment