Thursday 13 July 2017

Barabara kufungua ya Kasanga iwe fursa kwa wafanyabiashara

Na Gurian Adolf
Sumbawanga
WAFANYABIASHARA hapa nchini wameshauriwa kuanza kujipanga kufanya biashara katika nchi za Zambia,Burundi na Jamuhuri ya kidemokrasia ya Kongo mara tu ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kati ya Sumbawanga mjini na kuunganisha na Bandari ndogo ya Kasanga iliyopo mkoani Rukwa utakapo kuwa umekamilika.
Naibu  waziri wa ujenzi uchukuzi na Mawasiliano mhandisi Edwin Ngonyani aliyasema hayo jana wakati akiwa katika ziara ya kikazi akikagua  ujenzi wa barabara mbalimbali zinazojengwa kwa kiwango cha lami mkoani Rukwa.
Alisema kuwa hivi sasa kuna barabara inayojengwa kutoka mjini Sumbawanga kuelekea wilayani Kalambo mpaka kwenye bandari ndogo  ya Kasanga yenye urefu wa km 112  ambayo itafungua fursa ya mawasiliano baina ya nchi yetu na nchi hizo jirani.
Mhandisi Ngonyani alisema kuwa kwa kutumia njia ya majini yaani ziwa Tanganyika wafanyabiashara wataweza pia kusafirisha bidhaa zao na kuwapunguzia gharama na usumbufu ambao walikuwa wakiupata hapo awali.
Alisema kuwa kutokana na barabara hiyo kupita kwenye wilaya ya Kalambo pia itachochea maendeleo kwa wananchi kwani wataweza kufanya biasahara ndogo ndogo na za nyumba za kulala wageni kwakua madereva na abiria wengine watalazimika kulala katika mji wa Matai ambao ni makao makuu ya wilaya ya Kalambo sambamba na mji wa Kasanga wakati wakisubiri taratibu za kuruhusu mizigo  yao iweze kusafiriswa kwenda katika nchi hizo.
Naibu waziri huyo aliwaasa wakazi wa mji wa Matai  kujituma zaidi katika kuzalisha mazao ya chakula kwani barabara hiyo itapeleka neema kwao ambapo wataweza kuuza vyakula na kujipatia kipato kitakachowasaidia kuwekeza kwa maisha yao ya baadae sambamba na kuwasomesha watoto wao kwa kuwapa urithi wa elimu.
Kwa upande wake Sewede Kalimalwendo mkazi wa mji wa matai aliishukuru serikali kwa ujenzi wa barabara hiyo kwani kwa miaka mingi wamekuwa wakihangaika kutokana na kutokuwa na barabara ya uhakika.
Alisema kuwa barabara hiyo ya kiwango cha lami pamoja na kuwa bado haijakamilika lakini tayari wamepata manufaa makubwa ikiwemo ni pamoja na kushuka kwa gharama za nauri, kusafiri kwa muda mfupi sambamba na kuwezesha wafanyabiashara wengine wenye mitaji mikubwa kufika katika mji wao na hivyo kununua bidhaa kwa bei nzuri tofauti na hapo awali.
Aliwaomba pia wafanya biashara wengine wenye  uwezo kuwekeza viwanda katika wilaya ya Kalambo wafike katika wilaya hiyo kwani kuna fursa nyingi ambazo wataziona na uwekezaji wao utakuwa  na manufaa kwao wenyewe, wananchi na taifa kwa ujumla.
Mwisho

No comments:

Post a Comment