Tuesday 27 June 2017

Majambazi wateka kijiji, wapora

Na Walter Mguluchuma
Katavi
WAFANYABIASHARA wa kijiji cha Itenka Tarafa ya Nsimbo wilayani Mpanda mkoani Katavi wamelazimika kutimua mbio na kuyaacha maduka yao wazi baada ya kundi la Watu watano wanaosadikika kuwa majambazi kuvamia kijiji hicho nakupora mali  za wafanyabiashara  hao na kisha  kutokomea kusikojulikana.
Tukio hilo lilitokea  Juni 24 majira ya saa  1:30 za jioni ambapo watu hao walivamia kijiji hicho na kufanikiwa kupora fedha taslimu zaidi ya shilingi milioni  4 baada ya kuwatishia kwa kulipua milipuko ya baruti. 
Akitoa taarifa ya tukio hilo Kaimu  Kamanda wa  polisi Mkoa wa  Katavi Benedict  Mapujila  alisema majambazi  hao walifika  kwenye  eneo hilo  na  kuwavamia katika kijiji hicho na kisha kuanza kulipua  baruti  hewani  hali  iliyowafanya wafanyabiashara wa  maduka wakimbie na kuwacha  maduka yao yakiwa wazi.
Kaimu  Kamanda  Mapujila  alisema kuwa baaada ya wafanya biashara hao kuwa wamekimbia    ndipo majambazi hao  walipotumia mwanya huo kuingia ndani ya maduka  mawili na kupora kiasi cha  shilingi  4,300,000 na kisha kutokomea  zao.
Baada ya majambazi hao kukimbia ndipo wananchi wa  Kijiji  hicho walitoa taarifa kwa  jeshi la  Polisi juu ya tukio  hilo na polisi walifika  katika eneo hilo  baada ya  muda  mfupi na walianza  msako wa kuwasaka  majambazi hao hata  hivyo   hawakufanikiwa kuwakamata.
Alisema   polisi walifanya   uchunguzi kwenye  eneo la kijiji hicho na  hawakuweza  kufanikiwa kuokota  ganda lolote  la   lisasi hali iliyo ashiria kuwa   majambazi hao    hawakuwa na  bunduki bali walitumia  baruti  wakati wakitekeleza tukio  hilo.
Kaimu huyo wa kamanda alisema   hadi  sasa   kakuna mtu  yoyote aliye kamatwa  kuhusiana na tukio hilo na  jeshi la polisi  linaende na   msako  ili kuwakamata watu waliohusika kwenye tukio  hilo.
 Alieleza  kuwa  jeshi la  polisi limewaomba wananchi kutoa  ushirikiano kwa  jeshi la  polisi ili waweze kuwakamata watu hao na kuwa na tabia  ya kutoa  taarifa Mara tu uhalifu unapofanyika.
Mwisho

No comments:

Post a Comment