Saturday 27 May 2017

Wanaojifungulia nyumbani walalamikia kutozwa sh 50,000/-

Na Gurian  Adolf
Sumbawanga

BAADHI ya wanawake wa kata ya Lyangalile wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa wamelalamikia kitendo cha kutozwa fedha kiasi cha shilingi 50,000 kama adhabu kutokana na kujifungua katika eneo ambalo si salama na hakuna huduma za uzazi salama.

Wanawake hao walitoa malalamiko yao  kwa Katibu wa CCM mkoa wa Rukwa Mwanamasudi Msafiri Ibrahim Pazi alipokuwa katika kata hiyo akifanya ziara ya kukagua maendeleo ya chaguzi za ndani ya chama hicho na kusikiliza changamoto walizonazo wakazi wa kata hiyo.

Wakizungumza kwa malalamiko  wanawake hao walisema kuwa wamekuwa wakitozwa fedha hizo na watendaji wa afya pindi wanapofika katika vituo vya uzazi salama kwa lengo la kupata matibabu.

Mmoja wa wanawake hao aliyejitambulisha kwa jina la Marystella Kaputa mkazi  wa kata hiyo alisema kuwa wanaumia sana kwa kitendo cha kutozwa fedha hizo kama faini kutokana na kutojifungulia katika eneo ambalo  halitoi huduma za uzazi salama kama majumbani na njiani wanapokuwa wanapelekwa  kujifungua.

Alisema kuwa inawezekana nia ni njema ili kuwaadhibu wanawake ambao hawaendi kujifungua katika vituo vya huduma za uzazi salama lakini adhabu hiyo imekuwa  ni kubwa sana hasa  ikizingatiwa kuwa sio wote wanaofanya hivyo kwa makusudi bali  wengine wanajikuta inawatokea kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo ni pamoja na usafiri, maandalizi duni sambamba na ndugu zao kutofanya maamuzi wakati uchungu unapo waanza.

Naye Adelina Severino mkazi wa kata hiyo alisema kuwa kitendo wanachofanyiwa wanawake hao sio sawa bali  kinachotakiwa ni watendaji wa afya kuendelea kutoa  elimu ili wanawake waone umuhimu wa kwenda kujifungulia katika maeneo yanayotoa huduma za uzazi salama kama zahanati, vituo vya afya na hospitali ili kuepuka changamoto zinazoweza kuwakuta wakati wakijifungua katika maeneo hayo.

Kwa upande wake Sekunde Nanyumbu mkazi wa kata hiyo alisema kuwa wakati mwingine wanawake wanakutwa na hali hiyo kutokana na ndugu wa karibu kama mume, wakwe  na wengine wenye  maamuzi katika ukoo  kutowaruhusu ama kufanya maamuzi ya haraka ili wafike  katika maeneo yanayotoa huduma za uzazi salama na katika kata hiyo wanategemea zahanati iliyopo katika kijiji cha Katonto ambapo baadhi yao wanaishi umbali wa kilometa nne mpaka kuifikia zahanati hiyo hali ambayo imekuwa ikichangia wanawake kujifungua katika maeneo ambayo siyo salama kwao.

Hata hivyo katibu  huyo  wa ccm mkoa  wa Rukwa alilaani kitendo hicho na kuahidi malalamiko yao kuyafikisha kwa watendaji wa afya ngazi  ya mkoa  ili yashughurikiwe na kukomeshwa kabisa kwani mpaka sasa Sera ya afya ni huduma bure  kwa wakina mama wajawazito kitendo cha kuwa toza faini siyo sawa.

Baada ya rukwakwanza.blogspot.com kupata malalamiko hayo iliwasiliana na kaimu  mganga Mkuu wa mkoa  wa Rukwa Emmanuel Mtika alikiri kuwepo kwa malalamiko hayo na kusema kuwa wanaopaswa kupewa adhabu ni wanawake wanaojifungulia nyumbani ili waache tabia hiyo na si wale wanao jifungulia njiani lakini pia alisema  tume  imeundwa kwa lengo la  kuchunguza malalamiko hayo ili hatua ziweze kuchukuliwa kwani ni kosa kuwatoza faini hiyo ya shilingi 50,000 ambayo ni kubwa.

Mwisho

No comments:

Post a Comment