Sunday, 7 May 2017

Viongozi wa Madhehebu watakiwa kuwa chachu ya amani nchini

Na Gurian Adolf
Sumbawanga.
 
 Viongozi wa madhehebu ya dini nchini wametakiwa kutumia nyumba za ibada kama chachu ya kupatikana kwa amani endelevu katika jamii.

 Katibu wa Muungano wa Jamii Tanzania (MUJATA) Peter Kayemba Mpeleka alisema hayo wakati akizungumza na viongozi wa dini za kikristo kutoka makanisa mbalimbali ya mkoa wa Rukwa, kikao kilicholenga kuutambulisha muungano huo kilichofanyika katika ukumbi wa Kanisa la FPCT mjini hapa.

Katibu huyo alisema kuwa matukio ya mauaji yanayohusishwa na imani za kishirikina, ujambazi hata yale yasiyojulikana chanzo chake kama yanayotokea Ikwiriri mkoani pwani ni matokeo ya jamii kutokuwa na hofu ya mungu hivyo viongozi wa dini wana changamoto ya kuhakikisha jamii inapata amani muda wote.

Alieleza kusikitishwa na mauaji watu wasio na hatia yanayoendelea mkoani pwani, ambapo alitaka serikali kupitia vyombo vyake vya dola kuhakikisha vinadhibiti matukio hayo na mengine kadhaa yanayoripotiwa kutokea hapa nchini.

Akizungumzia mkoa wa Rukwa, Katibu huyo alisema ni jambo la kushangaza kuona matukio ya watu kupoteza maisha kwa imani za kishirikina bado yanatawala katika jamii wakati viongozi wa dini wapo na ni jukumu lao kuhakikisha wanatumia mimbali yao kuhubiri amani pasipo kuchoka.

"Sisi Mujata tumekuja hapa Rukwa kuwataka muanzishe kikundi cha muungano wa jamii Rukwa ambacho kitawakutanisha wananchi na viongozi wa dini ambao watatumia kama jukwaa la kukutana na kujadili mambo mbalimbali ikiwemo suala kupatikana kwa amani miongoni mwa jamii" alisema Mpeleka. 

Alisema kupitia MUJATA itazaliwa Muungano wa jamii mkoa wa Rukwa ( MUJARU) ambayo itakuwa na jukumu la kudhibiti uhalifu na vitendo vya kishirikina vinavyosababisha kutokea kwa mauaji ya mara kwa mara hasa katika maeneo ya vijijini.

Alisema jukumu la kudhibiti mauaji hayo si la vyombo vya dola pekee hivyo muungano huo ambayo viongozi wa madhebu ya dini watashirikishwa ndio itakuwa ni moja ya kazi zake.

Naye, Mchungaji Jacob Silungwe alisema viongozi wa dini wanaunga mkono wazo la mkoa huo kuanzisha muungano huo kwa kuwa hawaendi kinyume na sheria na taratibu za nchi.

Alisema pia wanatarajia utakuwa chachu ya kupatikana kwa amani na kupunguza si tu matukio ya mauaji ya kishirikina na uhalifu miongni mwa jamii.
Mwisho

No comments:

Post a Comment