Wednesday 31 May 2017

Vijana washauriwa kuacha pombe

Na Gurian  Adolf
Sumbawanga

BAADA ya serikali kupiga marufuku pombe aina ya viroba sasa vijana mkoani Rukwa wamehamia kunywa pombe inayoitwa WIN VODKA ambayo inahifadhiwa kwenye vichupa vya plastiki na inaingizwa nchini inayoonekana inatengenezwa nchini Malawi.

Pombe hiyo imechukua  umaarufu mkubwa kutokana na kuuzwa kwa bei ya shilingi 1,200 ambapo  ina ujazo wa mililita 200,na kiwango cha ulevi asilimi 42 ambayo vijana wengi  wakiwemo wanafunzi ndiyo wanatumia sana kilevi hicho.
Gazeti hili likifanya mazungumzo na baadhi ya vijana wanaotumia  kilevi hicho walisema kuwa wameamua kuanza kutumia kwakua kinauzwa kwa bei  naafuu na kinapatikana katika maeneo mbalimbali ya kuuzia vilevi.
Mmoja wa kijana huyo  Francis Januari alisema kuwa kwasasa imekuwa  ni ngumu kupata viroba na badala yake wameamua kunywa pombe aina ya Win Vodka ambayo imepata  umaarufu kwakua bei  yake ni chini  ya kiroba ambapo kabla ya kupigwa  marufuku viroba vya konyagi vilikuwa vikiuzwa kwa bei  ya shilingi 1,500.
Mwandishi wa gazeti hili alipita mtaani na kukuta kuna  mwanafunzi mmoja akilaumiwa na wenzake kuwa ameshindwa kuhudhuria shule baada ya kulewa  pombe aina ya Win Vodka na majirani wa mtoto huyo  walisema kuwa wanafunzi wengi  wanakunywa  pombe hiyo na kushindwa kuhudhuria vizuri shuleni. 

Hata hivyo gazeti hili likiweza kuwasiliana na mganga Mkuu wa hospitali ya mkoa  wa Rukwa Emmanuel Mtika ambapo alisema kuwa pombe daima huwa siyo sawa kwa matumizi ya afya ya binadamu bila kujali kiwango cha ulevi wala wapi inatengenezwa.

Alisema kuwa katika nchi yetu kuna  tasisi kama TBS pamoja na TFDA ambazo ndizo  zinajukumu la  kuhakiki  ubora na usalama  wa vyakula  na dawa kwa watumiaji  wa  hapa nchini na nivizuri  kuhakikisha wanatumia bidhaa ambazo zimethibitishwa na tasisi hizo.
Hata hivyo baada ya kufanya uchunguzi katika kifungashio cha pombe hiyo ya WIN VODKA ilibainika kuwa hakuna muhuri wa TBS wala TFDA ili kuthibitisha kuwa wamekihakiki kilevi hicho na iwapo kinafaa kwa matumizi hapa nchini.

Mwisho

No comments:

Post a Comment