Tuesday, 9 May 2017

Madereva wa serikali walalamika kudharauliwa na mabosi wao

Na Israel Mwaisaka
Sumbawanga

MWENYEKITI  wa chama cha Madereva mkoani Rukwa Peter konga amelalamikia kitendo cha baadhi ya madereva hao kudharauliwa na mabosi wao ikiwa ni pamoja na kutolipwa posho zao ama  kutotolewa kwa wakati ukilinganisha na zile zinazotolewa na maofisa wao wakati wao ndiyo wawezeshaji wa kuhakikisha maofisa wa serikali wanafika eneo husika na kutekeleza majukumu yao kwa wakati.

Alisema kuwa madereva wa serikali mkoani humo wamekuwa wakikabiliwa na changamoto nyingi kutoka kwa mabosi wao kiasi kwamba kutofurahia kazi hiyo na kuifanya bila amani kwani wakati wote wamekuwa wakitekeleza majukumu yao kwa hofu.

Akizungumza katika kikao cha mwaka cha madereva hao alisema kuwa wakati mwingine wanatumikishwa kufanya kazi ambazo hazimo hata katika majukumu yao ya ajira ikiwemo kutumwa majumbani kwa mabosi hao huku baadhi yao kuwasubiri katika baa na kumbi za starehe wakati wakifahamu fika sio wajibu wao kufanya hivyo.

Katika kikao hicho Madereva hao walimualika Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa Nyangi Msemakweli ambaye alikuwa ndiyo mgeni rasmi ambapo alisikitishwa na kilio cha madereva wa serikali mkoani Rukwa kwa kazi zao kutothaminiwa ipasavyo ikiwa ni pamoja na kupelekea halmashauri nyingi mkoani Rukwa kushindwa kupendekeza majina ya watumishi bora kwenye sherehe za Mei mosi mwaka huu.

Akiendelea kujibu risala ya madereva hao katika kikao kilichofanyika hivi karibuni kwenye ukumbi wa halmashauri ya mjini wa Sumbawanga juu ya kilio cha madereva kutothaminiwa kama watumishi wengine wa Umma mkurugenzi huyo alisema madereva wanafanya kazi kubwa katika kufanikisha utendaji wa majukumu ya serikali na kitendo cha madereva kutokuwemo kwenye utumishi bora amekubaliana kuwa sio sawa na kinawafanya wajihisi kama hawathaminiwi.

Alisema madereva wanafanya kazi kubwa na yeye kama mkurugenzi anaziona na kuwa sasa maazimio ya kikao hicho yataandikwa na kumpelekea katibu tawala wa mkoa na nyaraka nyingine ziende kwa Wakurugenzi wengine wa halmashauri zote za mkoa Rukwa ili kila mwajiri aweze kukiona kile kinacholalamikiwa na madereva hao.

Mkurugenzi huyo alidai kuwa haoni sababu za maofisa kuwadharau madereva bali na wao ni watumishi kama walivyo wao kwenye utumishi wa umma na kuwa hilo sasa wao kama viongozi watalichukua kwa uzito wa aina yake na kulizungumza katika vikao vyao.

‘’Madereva ni watumishi kama wengine na wote kazi zetu zinategemeana kwa nini wawepo watu wa kudharau kada nyingine hususani madereva na hili la uteuzi wa Wafanyakazi bora limedhihirisha ni jinsi gani kada hiyo inavyodharaulika na hili halikubaliki kamwe”....alisema

Mwakilishi wa katibu tawala wa mkoa Godfrey Haule kwa upande wake alidai kuwa licha ya madereva hao kuwa na malalamiko yao kwa mwajiri lakini na wao wana mapungufu kadhaa wanayotakiwa kujirekebisha ikiwemo la kutotunza siri za viongozo wao ikiwa ni pamoja na suala la utunzaji wa kumbukumbu (log book).

Alisema kuwa wakati serikali wanayafanyia kazi  mambo yao na wao watumie chama chao kuelekezana ukweli juu ya mapungufu yao na kuwa wakifanya hivyo ana imani kuwa mambo yatakwenda sawa na kufanikisha kazi za serikali kufanywa kwa usahihi.

Madereva wa serikali mkoani Rukwa wamekuwa wakifanya vikao vyao vya madereva kupitia chama chao ambapo wamekua wakizungumza mambo mbalimbali yanayowahusu wao na kutafuta haki zao pale wanapohisi kuonewa na kukiukwa.
mwisho

No comments:

Post a Comment