Sunday, 21 May 2017

Kituo cha afya Laela cha lalamikiwa kwa uchafu

Na Gurian Adolf
Sumbawanga
 
DIWANI wa viti maalumu wilayani Sumbawanga Omelina Mgawe amelalamikia hali ya kituo cha Afya cha Laela wilayani humo kuwa ni kichafu na kinahatarisha afya za wagonjwa na watu wanao wahudumiwa.
 Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga John Msemakweli      akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani.

Akizungumza katika kikao cha baraza la  madiwani wa halmashauri hiyo alisema kuwa kituo hicho cha afya hakiendani na misingi  ya afya bora, kitendo ambacho ni aibu kwani hata zahanati na vituo vya watu binafsi vinakuwa ni visafi kuliko vya serikali.

Alisema kuwa iwapo halmashauri hiyo isipofanya jitihada za kusafisha huenda hata kukaibuka magonjwa ambayo hayakuwepo kama kipindu  pindu na itakuwa ni fedheha kubwa kuona tasisi ya serikali ndio inahatarisha afya za wananchi.
Baadhi ya madiwani wakiwa katika kikao cha baraza la madiwani la halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga

Alimtaka mkurugenzi wa halmashauri hiyo kuchukua hatua kabla hali haijawa mbaya kupindukia kwani jamii haita  elewa iwapo tasisi ya serikali tena  kama ya afya ndiyo inakua chanzo cha mgonjwa wilayani humo.

Naye  Efraim  Konta diwani wa kata ya Zimba katika halmashauri hiyo alilalamikia kitendo cha kituo cha afya mtowisa kuwa na gari la  wagonjwa moja ambalo  licha ya kuwa linatumika katika shughuli nyingine lakini halitoshi kuwahudumia wakazi  wote wa halmashauri hiyo.

Alisema kuwa halmashauri hiyo ni kubwa na ina  idadi kubwa ya watu hivyo kuwa na gari moja bado ni changamoto kubwa kwani linashindwa kuhudumia halmashauri yote.
Baadhi ya wataalamu na wageni waalikwa wakiwa wanafuatilia kwa kina kikao cha baraza la madiwani la halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga

Akijibu malalamiko hayo mkurugenzi wa halmashauri hiyo John Msemakweli alisema kuwa suala la  usafi halina  mjadala ni lazima litekelezwe haraka kwani lipo  ndani ya uwezo wa halmashauri hiyo na kuhusu gari la  wagonjwa alisema jitihada zinafanyika kwaajili ya kupata gari jingine la  wagonjwa ambalo  litasaidia kuondoa kero iliyopo hivi sasa.

Aidha aliwaomba madiwani hao kama wanaweza kusaidia kutafuta wahisani wa nje na ndani watakao wezesha kupatikana gari la  wagonjwa ambalo  litasaidia kuwahudumia wananchi wa halmashauri hiyo.
 
Mwisho.

No comments:

Post a Comment